Na Sophia Kingimali.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametoa wito kwa vijana kuwa wazalendo na kukataa kutumiwa kwa malengo ya kisiasa na malengo binafsi ya watu wachache, badala yake walinde amani ambayo imeijenga Tanzania kuwa taifa linaloheshimika barani Afrika na duniani.
Wito huo ameutoa leo Disemba 2, 2025 wakati akizungumza na wazee wa Dar es Salaam, ambapo amesema Tanzania imejenga sifa ya kipekee duniani kutokana na utu, upole, ukarimu na umoja wa watu wake — misingi ambayo vijana wanapaswa kuilinda kama uti wa mgongo wa amani ya taifa.
“Sifa hii imeanza kushambuliwa na matukio ya vurugu yanayoratibiwa na watu wasiolitakia mema taifa, vurugu za Oktoba 29 na 30 ziliharibu mali, zikasababisha vifo, na kuvunja utamaduni wa upendo na ustaarabu unaowatambulisha Watanzania,” amesema Rais Samia.
Aidha ameongeza kuwa waliopoteza maisha na waliojeruhiwa ni Watanzania wenzetu, na hakuna aliye juu ya haki ya kuishi huku akisisitiza kuwa damu ya Mtanzania mmoja ikimwagika, taifa lote linaumia, hivyo kulinda amani ni wajibu wa kila mmoja.
Amesema vurugu hizo zilikuwa zimepangwa kwa malengo makubwa ya kisiasa na ziliratibiwa na watu waliotaka kutumia vijana kama chambo. Baadhi yao, amesema, walilipwa pesa ili washiriki maandamano bila hata kuelewa wanachodai.
Rais Samia alieleza kuwa uharibifu uliofanywa kuchoma vituo vya polisi, kuharibu miradi ya serikali, kuvamia biashara binafsi—hauwezi kuitwa maandamano halali, bali ni vurugu zilizoandaliwa kimkakati. “Maandamano ya kikatiba hayajawahi kuwa ya moto na mabomu ya petroli,” alisema.
Aidha, amehoji kwa nini vurugu zilipangwa siku ya uchaguzi, akieleza kuwa lengo lilikuwa kupotosha ukweli kuhusu mwelekeo wa matokeo huku akisisitiza kuwa serikali ilikuwa na wajibu wa kulinda maisha, mali na mipaka ya nchi kwa kutumia nguvu stahiki kulingana na tukio.
Rais Samia pia aliwakumbusha vijana kuwa ugumu wa maisha si sababu ya kuingia barabarani kuvuruga amani, akisema Watanzania wanapitia changamoto zinazofanana na za mataifa mengine na bado wengi wanahangaika kihalali kutafuta riziki zao.
Amesema tumejifunza kuwa vijana wengi hawana elimu ya uzalendo, ndiyo maana serikali imeunda wizara maalumu ya kushughulikia maendeleo ya vijana, ikiwa na mpango mkakati wa kuimarisha malezi ya kizalendo.
Kuhusu madai ya katiba mpya, Rais Samia ameeleza kuwa serikali haijayakataa, na tayari asilimia kubwa ya mapendekezo ya muda mfupi na wa kati yametekelezwa. Kazi iliyobaki ni ya muda mrefu ambayo mchakato wake utaendelea kwa utaratibu uliopangwa.
Amesisitiza kuwa tofauti za kisiasa hazipaswi kutumiwa kuhamasisha vurugu, kwani demokrasia inatoa nafasi ya kujadiliana, kutofautiana na kuendesha mashindano ya hoja bila kuvunja misingi ya nchi.
Aidha amewataka vijana kutokubali kutumika katika maandamano ambayo yanaendelea kuratibiwa na watu wa nje na ndani ya nchi, ambapo amesema serikali imejipanga vizuri kukabiliana na fujo zozote zitakazotokea huku akisisitiza nguvu itakayotumika itaendana na ukubwa wa tukio lenyewe.
“Nchi hii ni yetu sote, amani ni ngao yetu, na kizazi cha leo lazima kitete amani hii kama urithi wa thamani kwa vizazi vijavyo,” amesema.




