Na John Bukuku – Dar es Salaam
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema kuwa machafuko yaliyotokea nchini Tanzania ni matokeo ya mpango wa kutengeneza vurugu kwa madhumuni ya kuangusha dola nchini.
Aidha, amesema kuwa vijana walihamasishwa kushiriki machafuko hayo yaliyosababisha kusitishwa kwa masomo na kuleta madhara makubwa, hasa katika elimu ya juu. Amebainisha kuwa vurugu hizo zilikuwa sehemu ya mradi mpana uliofadhiliwa na watu wenye nia mbaya, na kwamba watekelezaji wa vurugu hizo wanapaswa kuchukuliwa hatua za kisheria. Akihutubia taifa leo Desemba 2, 2025, katika ukumbi wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, Dkt. Samia…
Aidha, Dkt. Samia amesema kuwa miradi ya serikali ikiwemo majengo, vituo vya mafuta, biashara binafsi na magari ya serikali imeathirika kutokana na machafuko hayo. Alifafanua kuwa maandamano ya kawaida ndani ya mfumo wa katiba yanaruhusiwa, lakini vurugu zilizotokea hazikuwa maandamano bali ni shambulio lililopangwa kwa makusudi.
Dkt. Samia amebainisha sababu za machafuko kuanza siku ya uchaguzi na kueleza kuwa serikali ililazimika kutumia nguvu kulinda usalama wa raia na mali zao.
Aidha, amesema kuwa nguvu iliyotumika ilikuwa sawia na kiwango cha tukio lililojitokeza, huku akibainisha kuwa waandamanaji walijaribu kufanya mapinduzi ambayo hayakufanikiwa.
Dkt. Samia amesema kuwa waandamanaji wengi walijiandaa njiani, na serikali ilichukua hatua stahiki za kuzuia hali kuharibika zaidi.
Aidha, amesema kuwa nguvu iliyotumika ilikuwa ni sehemu ya juhudi za kulinda amani na mipaka ya nchi.
Pia, amebainisha kuwa katika uchaguzi uliofanyika, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilipata ushindi mkubwa kwa sababu wananchi walitambua kazi iliyofanywa na chama hicho.




