John Bukuku na Meleka Kulwa, Dodoma
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametoa wito kwa vijana na Watanzania kwa ujumla kulinda amani ya nchi, akisisitiza kuwa misingi ya ustawi wa Taifa imejengwa juu ya utulivu na umoja.
Akihutubia Ijumaa ya Novemba 14, 2025 jijini Dodoma, wakati wa ufunguzi wa Bunge la 13, Rais Samia amebainisha kuwa:
“Nchi hii imejengwa kwenye misingi ya amani na utulivu wa kisiasa. Sisi wazazi wenu tungeshawishika kuyafanya mliyoyafanya wakati huu, nchi hii isingekuwa na neema na maendeleo mnayoyaona leo.”
Ameonya vijana kuepuka vitendo vya uhalifu vinavyoweza kuhatarisha Taifa, akisema:
“Nchi hii ni yenu. Kwa shida zozote zile zinazowakabili, msikubali hata siku moja kushawishiwa kuichoma nchi yenu wenyewe. Msikubali kukata tawi la mti ambalo mmeukalia.”
Rais Samia pia amesema vijana wengi waliokutwa kwenye makosa ya uhaini hawakujua wanachokifanya, na kueleza kuwa anatoa msamaha wa kisheria kwa wale waliokutwa walifuata mkumbo.
“Ninatoa msamaha huo kwa sababu hata maneno ya Mungu katika Luka 23:34 yanasema: ‘Baba uwasamehe kwa kuwa hawajui watendalo.’”
Amehimiza umuhimu wa maelewano na umoja kwa Taifa, akisema:
“Niwasihi sana Watanzania tuongozwe na dhamira ya maelewano, ushirikishwaji, kujirekebisha, na umoja.”
Amesema Serikali itaendelea kuimarisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, akibainisha kuwa ni tunu inayopaswa kulindwa na kuendelezwa.
Kwa upande wake, Ali Hamad, mzaliwa wa Songea na mkazi wa Magole wilaya ya Ilala Dwr es Salaam fundi magari mtaa wa Libya , akizungumzia juu ya hotuba ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema maandamano yaliyofanyika hayakuwa halali na kwamba kuchoma sheli, kuvamia maduka ya watu na kuchoma magari barabarani si maandamano halali bali ni uhalifu. Amesema:
“Mimi sipo kwenye chama. Mimi sio Chadema wala sio CCM, bali nazungumzia uasilia wangu wa mimi mwenyewe. Ninachowaomba vijana wenzangu, tusifuate mikumbo au muamko.”
Ameongeza kuwa maandamano hayo yamesababisha maafa makubwa kwa ndugu zetu kupoteza maisha, watoto shuleni kupata usumbufu wa usafiri. Amesema wanafunzi walishindwa kwenda shule kwa wakati, daladala hazikufanya kazi kama kawaida, na baadhi ya watoto hawakurudi nyumbani kwa wakati.
Amesema maandamano halali hutakiwa kuwa na kibali cha serikali, na polisi huongoza maandamano hayo. Ameonya vijana kutorudia tabia hizo kwa kuwa zimeathiri watu wengi, ikiwemo biashara kufilisika kutokana na uharibifu wa mali.
“Nyanya zilizuliwa kuingia sokoni, zilizokuwa sokoni zimeoza zote na watu wamefilisika kwenye biashara zao—wameibiwa kila kitu na Serikali imeingia hasara.” amesema Ali Hamad.
Amesema kundi kubwa lililoshiriki maandamano lilikuwa la vijana wadogo ambao hawajajua maisha, na kwamba hata Rais alisema anaweza kuwasamehe waliokutwa na makosa madogo baada ya kushawishiwa.
“Sijamwona mzee; ni zaidi ya vijana wadogowadogo. Ni muhemko wa vijana ambao bado hawajui maisha ni nini.” amesema Ali Hamad.
Amebainisha kuwa eneo lao la Magole halikupata madhara yoyote kutokana na kufuata maagizo ya serikali ya kukaa nyumbani mpaka kutangaziwa.
“Hakuna mtu aliyefariki. Kila mtu alikuwa amekaa nyumbani akifanya shughuli zake.” amesema Ali Hamad.
Amesema kuwa kutii amri ya serikali ni muhimu, na hakuna askari aliyempiga mtu bila sababu na hata waliopata madhara ni matokeo ya maandamano hayo ambayo yaliambatana na uhalifu ndani yake.
Amebainisha kuwa wananchi wengi waliathirika kiuchumi, ikiwemo huduma za mtandao kusimama na shughuli za Tigo Pesa kushindwa kufanyika Benki ziliathirika. Hivyo, amewataka Watanzania kuwa na subira na kuepuka kufuata matamko ya mitandaoni.
“Hao wanaohamasisha maamdamano Sijaona taarifa yao hata moja ikisema, ‘Watanzania nimewatumia mafuta ya kula’… Sisi Watanzania tupeane taarifa, tupeane elimu sisi wenyewe kuepuka matukio mabaya yanayoweza kuathiri taifa letu.” amesema Ali Hamad.
Ametoa wito kwa vijana kujituma na kutokata tamaa, akisisitiza kuwa hakuna Rais atakayewaletea chakula nyumbani bali kuweka miundombinu ya kuwasaidia kufika kazini na kufanya shughuli za kiuchumi ili kunipatia kipato
“Jitume kijana mwenzangu, usikate tamaa. Hakuna Rais atakuletea ugali nyumbani. Anakuwekea miundombinu.” amesema Ali Hamad.

