Na Silivia Amandius.

Muleba,Kagera.

Mgombea Ubunge wa Jimbo la Muleba Kaskazini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Adonius Bitegeko, ameweka historia kwa kufunga kampeni zake kwa mkutano mkubwa uliohudhuriwa na maelfu ya wananchi kutoka kata mbalimbali za jimbo hilo. Mkutano huo ulifanyika kwa shamrashamra na hamasa kubwa, huku wananchi wakionesha imani yao kwa sera na utekelezaji wa CCM katika kuwaletea maendeleo endelevu.

Akihutubia wananchi, Bitegeko aliwaahidi kuwa endapo watampa ridhaa ya kuendelea kuliongoza jimbo hilo, atahakikisha ahadi zote zilizopo kwenye Ilani ya CCM zinatekelezwa kwa vitendo. Amesema vipaumbele vyake vitakuwa kuimarisha huduma za afya, elimu, miundombinu ya barabara na kuinua kipato cha wananchi kupitia miradi ya kilimo, uvuvi na ujasiriamali.

Kampeni hizo zimefungwa rasmi Oktoba 25 mwaka huu katika kata ya Katoke, ambapo viongozi mbalimbali wa chama walihudhuria akiwemo Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kagera, Nazir Karamagi, pamoja na Mwenyekiti wa UVCCM mkoa huo, Farisi Buruhani. Hafla hiyo ilihusisha burudani, hamasa, na wito wa kudumisha umoja na mshikamano miongoni mwa wanachama wa CCM na wananchi kwa ujumla.

Akizungumza wakati wa mkutano huo, Mwenyekiti wa Vijana Mkoa wa Kagera, Farisi Buruhani, aliwataka vijana kutokubali kutumika kama chanzo cha vurugu, akisisitiza kuwa taifa bila vijana ni taifa lisilo na mwelekeo. Aliwahimiza vijana kuitunza amani ya nchi na kushiriki kikamilifu katika uchaguzi mkuu ujao kwa amani na utulivu.