NA JOHN BUKUKU- ILALA
Kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Peter Msigwa, amempongeza Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa anayoifanya kuwaletea Watanzania maendeleo katika sekta mbalimbali.
Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika kwenye uwanja wa Kecha, Kinyerezi wilayani Ilala, mkoa wa Dar es Salaam Oktoba 22, 2025, Msigwa amesema kuwa yeye pamoja na mgombea mwenza wamezunguka nchi nzima na kujionea namna wananchi wanavyokiunga mkono Chama Cha Mapinduzi.
Amesema kuwa Tanzania ni nchi nzuri ambayo imejaliwa amani na utulivu, na kwamba changamoto zinazojitokeza katika baadhi ya maeneo hazimaanishi kuwa serikali haijali. Aidha, amebainisha kuwa Serikali ya Dkt. Samia imegusa katika kila sekta ikiwemo kilimo, afya, barabara na ajira kwa vijana.
Pia, amesema kuwa maendeleo ni mchakato unaohitaji umoja na mshikamano, na kuwataka Watanzania kuendelea kushikamana kwa pamoja kumuunga mkono Dkt. Samia na CCM ili kuendeleza mafanikio yaliyopatikana.
Aidha, amesema kuwa takwimu zinaonyesha wazi kuwa Tanzania inasonga mbele katika nyanja zote, na kwamba ni wakati wa Watanzania kutumia kura zao kuimarisha msingi wa maendeleo badala ya kugawanyika kwa mambo yasiyo na msingi.
Msigwa amebainisha kuwa utekelezaji wa Ilani ya CCM umefanyika kwa kiwango kikubwa na kwa ujasiri, na kwamba dira ya maendeleo ya mwaka 2050 inaonyesha matumaini makubwa kwa taifa.
Amesema kuwa ni ukweli usiopingika kuwa barabara za lami, vituo vya afya, shule, madaraja na bei za mazao kama pamba na kahawa zimeendelea kuimarika, hali inayoonyesha dhamira ya kweli ya Serikali ya kuwatumikia wananchi.
Aidha, amebainisha kuwa Dkt. Samia ameendeleza falsafa ya waasisi wa taifa kwa kuthibitisha kuwa kilimo ni uti wa mgongo wa uchumi, na ameonyesha hilo kwa vitendo kupitia miradi mikubwa ya maendeleo inayoendelea kote nchini.
Pia, Msigwa ametoa wito kwa Watanzania kuwa wavumilivu na wenye subira, akibainisha kuwa serikali itaendelea kushughulikia changamoto chache zilizopo huku ikiimarisha mafanikio yaliyopatikana.



