NA JOHN BUKUKU- DAR ES SALAAM

Baada ya kufanya mikutano mikubwa katika mikoa ya Pwani na Rukwa, leo Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuhitimisha kampeni zake za wiki hii jijini Dar es Salaam kupitia mkutano mkubwa wa hadhara katika Wilaya ya Kinondoni.

Wananchi wa jiji la Dar es Salaam, hususan wakazi wa Kinondoni, wamejitokeza kwa wingi kuandaa mapokezi makubwa ya kumpokea Dkt. Samia, ambaye amekuwa akipita nchi nzima akieleza mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita na kuomba ridhaa ya kuendeleza kazi hiyo kupitia ilani ya CCM ya mwaka 2025–2030.

Kwa mujibu wa maandalizi ya chama, mkutano huo unatarajiwa kuvutia maelfu ya wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya jiji, ukiwa ni fursa kwa mgombea huyo kuelezea kwa kina mipango ya maendeleo ya miji mikubwa, ikiwemo Dar es Salaam, katika kipindi kijacho.

Miongoni mwa mambo anayotarajiwa kugusia ni pamoja na kuboresha huduma za kijamii, kupunguza msongamano wa magari, ujenzi wa makazi bora ya wananchi wa kipato cha chini, pamoja na kuimarisha ajira kwa vijana na wanawake.

Aidha, Dkt. Samia amekuwa akisisitiza umuhimu wa kudumisha amani, umoja na mshikamano wa kitaifa, akiwahimiza Watanzania wote kujitokeza kwa wingi kupiga kura Oktoba 29, na baada ya kupiga kura kurudi majumbani kwa amani wakisubiri matokeo, bila vurugu wala taharuki.

Kauli mbiu inayotumika katika mikutano yake ni “Tunaendelea na Mama hadi 2030”, ikibeba ujumbe wa matumaini na mwendelezo wa maendeleo endelevu chini ya uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan.