NA JOHN BUKUKU- MUGUMU SERENGETI

Mgombea urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, amehimiza umuhimu wa mshikamano wa Watanzania bila kujali jinsia, kabila au mila, akisisitiza kuwa maendeleo ya taifa yanatokana na ushirikiano wa wanawake na wanaume katika kulijenga taifa.

Amesema kuwa maendeleo endelevu hayawezi kupatikana bila umoja na ushirikiano kati ya wanaume na wanawake, kwani wote wamepewa uwezo sawa na Mungu katika kufikiri na kutenda.

“Maendeleo ya nchi yanategemea ushirikiano kati ya wanaume na wanawake, na kwamba wote wamepewa uwezo sawa na Mungu katika kufikiri na kutenda,” alisema Dkt. Samia.

Ameongeza kuwa wanawake wana uwezo wa kufanya kazi sawasawa na wanaume, hivyo Tanzania itaendelea kujengwa kwa nguvu za umoja wa wananchi wote bila ubaguzi.

Aidha, Dkt. Samia amesema Serikali itaendelea kuimarisha sekta za elimu, afya, maji, kilimo na miundombinu kupitia utekelezaji wa Ilani ya CCM. Amesema dhamira ya Serikali ni kuhakikisha huduma za elimu zinawafikia Watanzania wote, ikiwemo elimu ya msingi, sekondari, vyuo vya ufundi (VETA) na vyuo vikuu.

Katika huduma za afya, Dkt. Samia amesema Serikali inalenga kuhakikisha kila Mtanzania anakuwa karibu na huduma hizo katika ngazi zote, kuanzia zahanati hadi hospitali za rufaa. Amesema kuwa katika Mkoa wa Mara tayari Serikali imejenga Hospitali ya Rufaa na itaendelea kuijengea uwezo zaidi sambamba na kuimarisha vituo vya afya na zahanati.

Ameongeza kuwa katika sekta ya maji, Serikali inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali kuhakikisha kila mkazi wa Serengeti anapata huduma ya maji safi na salama, sambamba na kupeleka umeme katika vitongoji vyote vya Mkoa wa Mara baada ya kukamilisha usambazaji vijijini.

Kuhusu sekta ya kilimo, Dkt. Samia amesema Serikali itaendeleza ruzuku, kutafuta masoko ya bidhaa za kilimo na kuboresha mazingira ya uzalishaji, huku wakulima na wafugaji wakipatiwa fursa zaidi za kuinua kipato chao.

Mwisho, Dkt. Samia amewataka wananchi wa Serengeti na Mkoa wa Mara kwa ujumla kuendeleza mshikamano huo wa wanawake na wanaume kwa kuwachagua wagombea wa CCM katika ngazi zote, ili kuleta maendeleo endelevu katika maeneo yao.