NA DENIS MLOWE, IRINGA
ALIYEKUWA mbunge wa Iringa Mjini Jesca Msambatavangu amewapigia magoti mamia ya wananchi wa kata ya Kihesa kujitokeza kwa wingi kumpigia kura Mgombea urais wa Tanzania kwa tiketi ya CCM Dk. Samia Suluhu Hassan, Mgombea ubunge wa jimbo la Iringa mjini Fadhili Ngajilo na diwani kata ya Kihesa Hosea Kabelege Oktoba 29.
Akielezea kwanini watu wajitokeze kwa wingi Oktoba 29, Msambatavangu alisema kuwa suala la kwanza ni katiba inataka hivyo tunatakiwa kufanya uchaguzi kila baada ya miaka 5 hivyo uchaguzi huu muhimu kwa kila mwananchi kujitokeza kupiga kura kuichagua CCM kwa mengi ambayo yamefanyika nchini.
Alisema kuwa kutokana na katiba kutaka kila baada ya miaka 5 kufanyike uchaguzi rais mama Samia Suluhu Hassan kwa aliapa kuilinda kuhakikisha yale ambayo yako kwenye katiba yanatatekelezwa na ndio maana 29 tukapige kura.
Msambatavangu alisema kuwa suala la pili kwanini tukapige kura ni maendeleo katika sekta mbalimbali ikiwemo miradi ya afya, elimu, miundo mbinu kila mmoja shahidi katika hilo.
“Tukapige kura tuwachague wagombea wa chama cha mapinduzi kwani kimejipambanua kushughulika na changamoto za wananchi na wawakilishi wake ni wagombea wa Ccm ambao wamekamilika kila idara katika kuongoza na kuwaletea maendeleo wananchi” Alisema
Kwa upande wake mgombea ubunge Jimbo fa Iringa Mjini kupitia CCM, Fadhili Ngajilo alisema kuwa kupitia ilani ya CCM akichaguliwa atalivalia njuga suala la njia mchepuko (bypass) ya Igumbilo kupitia Chuo cha Iringa ambayo inapita kata ya Kihesa kuanza kutumika mara ya kupasuliwa mlima ianze kuzoeleka na kusogeza uchumi wanakihesa.
Aidha alisema kuwa watahakikisha wanajenga barabara kutoka Nduli hadi Chuo Kikuu cha Iringa kuchochea maendeleo zaidi kwa kiwango bora kabisa na kuhakikisha kwamba mara baada ya miradi hiyo kukamilika watajenga Stendi ndogo ya magari ya kwenda Dodoma kuepuka kufanya mabasi kupaki barabarani maeneo ya kata Kihesa
Aidha alisema kuwa atahakikisha Makundi yote ya vijana yako katika mipango maalum wa kupata elimu ya madini kwani mkoa wa Iringa una madini ya kutosha.
Ngajilo aliongeza kuwa mradi wa Kihesa Kilolo utatumika vyema kuchangamsha hivyo kwa kushirikiana na diwani watahakikisha inatekelezwa na hiyo iko kwenye ilani ya uchaguzi.
Kuhusu michezo alisema kuwa atatamani kuona Kihesa inajishughulisha na mambo ya michezo na kuirudisha timu iliyotamba miaka hiyo ya Kihesa stars na kuhakikisha vipaji vinazalishwa.
“Hivyo tushikamane na tushirikiane katika kuleta maendeleo ya kata na jimbo kwa ujumla na tutashughulika na changamoto ya mtu mmoja moja katika ujasiriamali Vijana wote. Kina mama na wananchi wote” Alisema.
Diwani Mteule wa Viti maalum Kata ya Kihesa anayesubiri kuapishwa Sara Ponela aliungana na Jesca Msambatavangu kuomba wananchi wajitokeze kwa wingi Oktoba 29 kukipigia kura chama cha Mapinduzi.
Sara Alisema kuwa wananchi wa Iringa wanajua pumba na mchele ni upi hivyo watajitokeza kwa wingi kama ilivyo desturi katika kupiga kura za Rais kwa kishindo na kuongoza kwa mikoa yote.

