Katibu Mkuu mstaafu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dkt.Bashiru Ally akizungumza kwenye uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza na kuwasihi wananchi kuwa na Imani thabiti kwa mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu kutokana na kuwa na utendaji kazi uliotukuka hususani katika kuwaletea wananchi maendeleo.
…………..,
NA JOHN BUKUKU, MWANZA
Katibu Mkuu mstaafu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dkt.Bashiru Ally amewasihi wananchi kuwa na Imani thabiti kwa mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu kutokana na kuwa na utendaji kazi uliotukuka hususani katika kuwaletea wananchi maendeleo.
Akihutubia katika viwanja vya Nyamagana Mkoani Mwanza Oktoba 08, 2025, Dkt Bashiru alisema mgombea Uraias amekabiliana na majaribio makubwa na akaonyesha uwezo wake wa kuyakabili na kuyatatua hivyo aliwasihi wananchi wawe na imani na uongozi wake kabla ya uchaguzi unao karibia.
Dkt Bashiru alisema kwamba umoja wa kitaifa, amani na utulivu lazima ulindwe kila wakati pia aliwakumbusha wapiga kura kwamba Tanzania ilibaki imara hata wakati wa kifo cha ghafla cha Rais John Magufuli, wakati Samia alipochukua uongozi wa taifa.
“Kama nchi yetu imeendelea kuwa na umoja, kama CCM imeendelea kuwa imara, na kama amani na usalama vimeendelea kutawala wakati wa mabadiliko ya ghafla, basi ni wazi kuwa tupo salama chini ya uongozi wake,” alisema.
Aidha, alilaani vikali sauti zinazojaribu kuchochea chuki na machafuko ambapo alieleza hizi ni kelele zinazochochewa na wachache hivyo tusikubali kabisa kuvuruga amani y nchi yetu.
Alisema hatupaswi kupoteza umakini hatupaswi kuhamasisha chochote kinachotuchukua nje ya mstari wetu wa kujenga taifa.
“Watanzania tunapaswa kuendelea kuwa na umoja na si kuruhusu chuki na fitina kuingia nchini,” alisisitiza Dk. Bashiru. Pia aliwatambua vijana kwa kuwa sehemu muhimu ya taifa na kuwahamasisha kuendelea kuwa na msimamo wa kulinda umoja wa nchi.

