NA JOHN BUKUKU -BABATI MANYARA
Muendelezo wa kampeni za Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, unatarajiwa kuendelea leo mkoani Manyara kwa kufanya mkutano mkubwa wa kampeni mjini Babati.
Rais Dkt. Samia anawasili Babati baada ya mikutano mikubwa aliyofanya jana katika majimbo ya Karatu, mkoani Arusha, na Katesh, wilayani Hanang, mkoani Manyara, ambapo alihutubia maelfu ya wananchi waliomlaki kwa shangwe na hamasa kubwa.
Katika hotuba zake, Dkt. Samia aliwaahidi wananchi kuendeleza juhudi za kukuza uchumi kupitia sekta mbalimbali zikiwemo kilimo, miundombinu, afya na elimu. Akiwa Katesh, aliweka msisitizo maalumu katika kuboresha zao la ngano pamoja na kusaidia wananchi wa Hanang waliokumbwa na maafa ya maporomoko ya tope kwa kuwajengea makazi salama.
Leo mjini Babati, Rais Samia anatarajiwa kuzungumzia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwa kuainisha miradi mikubwa inayotekelezwa na itakayotekelezwa mkoani Manyara, ikiwemo sekta ya barabara, maji, elimu na kilimo, ili kuongeza tija na kuinua hali ya maisha ya wananchi.
Wananchi wa Babati na vitongoji vyake wamejipanga kwa wingi kumpokea kwa shamrashamra, huku viongozi wa CCM mkoani humo wakieleza kuwa mkutano huo utakuwa wa kihistoria na utadhihirisha mshikiano wa wananchi na chama hicho kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 29.
