Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan leo October 03,2025. akimkabidhi ilani ya uchaguzi Mgombea Ubunge wa Jimbo la Hanang Asia Halamga mbele ya wananchi waliofurika kwenye Mkutano wa Kampeni uliofanyika uwanja wa Steandi ya Mabasi mjini Katesh Having. 

………… 

NA JOHN BUKUKU- KATESH, MANYARA

Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, amepokelewa kwa shangwe kubwa na wananchi wa Kata ya Katesh, Wilaya ya Hanang, Mkoani Manyara, ambapo alihutubia maelfu ya wakazi waliojitokeza kumsikiliza katika Uwanja wa Stendi ya Mabasi Katesh.

Wananchi walijitokeza kwa wingi, wakiwa na mabango, nyimbo na vigelegele, hali iliyodhihirisha mapenzi makubwa kwa Rais Samia, ambaye ameendelea kuvutia heshima na upendo wa wananchi kutokana na utendaji wake wa kazi na sera zake za maendeleo.

Akizungumza katika mkutano huo wa kampeni, Rais Dkt. Samia alitumia nafasi hiyo kugusia maafa yaliyosababishwa na maporomoko ya tope yaliyotokea Hanang mwishoni mwa mwaka jana na kusababisha vifo vya watu kadhaa na uharibifu mkubwa wa mali.

Alisema Serikali yake ilichukua hatua za haraka kusaidia waathirika wa janga hilo kwa kuwapatia misaada ya kibinadamu na kuanzisha mpango wa ujenzi wa makazi mapya kwa familia zilizopoteza makazi. Rais Samia alieleza kuwa amefanya uamuzi wa kuhakikisha waathirika wa maporomoko ya tope wanapewa makazi salama na yenye huduma stahiki ili kurejesha maisha yao katika hali ya kawaida.

“Leo nikiwa hapa Katesh, napenda kurudia kutoa pole kwa familia zilizopoteza ndugu zao katika janga la maporomoko ya tope. Serikali yenu itaendelea kushirikiana nanyi kuhakikisha tunajenga upya maisha yenu na kuimarisha miundombinu ili maafa kama haya yasilete madhara makubwa tena,” alisema Rais Samia.

Aidha, alibainisha kuwa Serikali imejipanga kuimarisha mifumo ya tahadhari ya majanga, sambamba na kuwekeza zaidi katika miradi ya maendeleo, ili wananchi wa Hanang na maeneo mengine nchini waweze kuishi kwa usalama na ustawi.

Katika hotuba yake, Rais Samia pia alimsifia Mgombea Ubunge wa Jimbo la Hanang, Kea, akisema ameeleza kwa kina maendeleo ya ukarabati wa miundombinu ya Katesh yanayoendelea vizuri kwa lengo la kuurejesha mji huo katika hali yake ya awali baada ya maafa ya maporomoko ya tope.

Mkutano huo ulifanyika katika shamrashamra kubwa, ambapo wananchi walionyesha mshikamano wao kwa CCM na kumhakikishia Rais Samia kuwa watajitokeza kwa wingi kumpigia kura katika uchaguzi wa Oktoba 29.

Sehemu ya wananchi wa Katesh
waliohudhuria mkutano wa hadhara wa Kampeni za Uchaguzi kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) uliofanyika Wilayani Hanang mkoani Manyara tarehe 03 Oktoba, 2025.