NA JOHN BUKUKU- KATESH, MANYARA

Waziri Mstaafu na Mbunge wa Zamani wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu, amewataka Watanzania kujitokeza kwa wingi Oktoba 29 kushiriki uchaguzi kwa kumpigia kura Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), ili kuonesha heshima kwa kazi kubwa alizozifanya katika kipindi cha uongozi wake wa awamu ya sita.

Akizungumza kwenye mkutano wa kampeni wa Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan, uliofanyika kwenye Uwanja wa Stendi ya Katesh, Wilaya ya Hanang mkoani Manyara, Nyalandu alisema Rais Samia ameleta mageuzi makubwa nchini katika muda mfupi, hususan katika sekta za afya, elimu, maji na miundombinu ya barabara.

“Mama ameibadilisha Tanzania kwa muda mfupi sana. Amefanya mambo mengi ya maendeleo ambayo kila mmoja anaweza kuyaona. Sasa ni wakati wetu wa kumrudishia heshima kwa kwenda kupiga kura Oktoba 29,” alisema Nyalandu.

Aliwataka Watanzania kupuuza propaganda na makundi ya watu wanaotaka kuwavunja moyo wasishiriki uchaguzi huo, akisema ni wajibu wa kila Mtanzania kutumia haki yake ya kidemokrasia kwa kuchagua viongozi bora.

“Tusiwaache wagonjwa nyumbani. Kama kuna mtu hawezi kutembea, tumsaidie. Tuondoke wote kwenda kupiga kura, tumheshimu Rais wetu mpendwa Dkt. Samia,” alisisitiza.