NA JOHN BUKUKU- HANANG, MANYARA
Mbunge wa zamani na Waziri, Lazaro Nyalandu, akizungumza kwenye mkutano wa kampeni wa Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, uliofanyika katika Uwanja wa Stendi ya Katesh, wilayani Hanang mkoani Manyara, Oktoba 3, 2025, amesema kuwa Rais Samia amekuwa mstari wa mbele kugusa maisha ya wananchi katika nyakati za majanga na mahitaji makubwa.
Amesema kuwa alipokuwa Waziri, aliwahi kushuhudia jinsi Dkt. Samia, akiwa Makamu wa Rais, alivyojitoa kuwafariji wafiwa na manusura wa ajali ya Shule ya Lucky Vincent, ajali iliyosababisha vifo vya wanafunzi 30 na kujeruhi watatu.
Amebainisha kuwa Dkt. Samia alihusika binafsi kupitia uhusiano wake kuhakikisha watoto hao watatu wanapelekwa Marekani kwa matibabu ya kibingwa, wakifanyiwa upasuaji mkubwa wa mifupa na uti wa mgongo, hali iliyowawezesha kupona na sasa wanasoma vyuo vikuu.
Aidha, ameeleza kuwa katika tukio la tetemeko la ardhi lililotokea Katesh, Mama Samia akiwa Rais alifika binafsi kuwatembelea majeruhi, kutoa faraja kwa familia zilizopoteza ndugu zao na kuhakikisha serikali inabeba gharama za mazishi kwa heshima.
Pia, Lazaro amesema kuwa hatua hizo ni kielelezo cha dhamira ya Dkt. Samia kuimarisha sekta ya afya nchini, ikiwemo kujenga mtandao wa vituo vya afya vilivyo na madaktari, wauguzi na mabingwa hata ngazi ya wilaya.
Aidha, ameongeza kuwa hali ya huduma za afya nchini imeboreshwa kwa kiwango kikubwa ukilinganisha na miaka ya nyuma, hatua iliyosaidia kuokoa maisha ya Watanzania wengi.
Vilevile, amebainisha kuwa Dkt. Samia amefanya uboreshaji mkubwa wa huduma za maji vijijini, jambo lililopunguza magonjwa yanayotokana na ukosefu wa maji safi na salama, huku pia akitoa fursa nyingi kwa vijana kushiriki katika shughuli za kiuchumi na maendeleo.
Aidha, ametoa wito kwa wananchi wa Manyara na Watanzania kwa ujumla kumpigia kura ya ndiyo Dkt. Samia katika uchaguzi mkuu ujao, akibainisha kuwa ni njia ya kulinda amani ya nchi na kuendeleza kasi ya maendeleo iliyofikiwa katika kipindi cha uongozi wake.


