NA JOHN BUKUKU – MOSHI

Aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Vunjo, Mkoani Kilimanjaro, Charles Kimei, amemshukuru Mgombea wa Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuwajali wananchi wa jimbo hilo kwa kuwapatia shilingi bilioni 51 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Akizungumza na mwandishi wetu leo, Oktoba 1, 2025, mkoani Kilimanjaro kuhusu maendeleo yaliyofanyika chini ya uongozi wa Dkt. Samia, Kimei amesema kuwa kati ya mwaka 2010 hadi 2020, Rais Samia alitoa jumla ya shilingi bilioni 21 kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo katika Jimbo la Vunjo.

Ameeleza kuwa katika kipindi hicho, Rais Samia ameonyesha dhamira ya dhati ya kuwaletea wananchi maendeleo kupitia miradi ya kijamii na kiuchumi, ikiwemo utoaji wa mikopo kwa vijana na kuanzisha fursa za ajira.

“Rais Samia amekuwa mtu wa kujali sana wananchi wake, na amekuwa mstari wa mbele katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo yenye kuleta tija kwa jamii,” amesema Kimei.

Amewataka Watanzania kushiriki kikamilifu katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu na kumpiga kura ya ndiyo ili aendelee katika nafasi ya urais kwa ajili ya kuleta maendeleo kwa Taifa.