Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
Mwakilishi wa Jimbo la Pangawe kupitia Chama cha ACT-Wazalendo, Ndg. Omar Said Shaaban ameendelea kupata mwitikio mkubwa wa wananchi, huku akiwasihi wakaazi wa jimbo hilo kujitokeza kwa wingi Oktoba mwaka huu kuhakikisha wanalinda kura na kufanya ushindi kuwa halisi.
Akizungumza katika mikutano ya kampeni, Omar Shaaban alisema wananchi wa Pangawe wameonyesha dhamira thabiti ya kutaka mabadiliko ya kweli kupitia ACT-Wazalendo, chama kinachopeperusha bendera ya matumaini na dira mpya ya Zanzibar.
“Sisi ni washindi, na tutashinda. Huu ndio wakati wa kuhakikisha tunalinda kura zetu na kuilinda demokrasia ya nchi yetu. #LindaKura si kauli mbiu tu, bali ni wajibu wa kila mmoja wetu,” alisema Omar.
Wananchi wa maeneo mbalimbali ya Pangawe walimpongeza kwa dhamira yake ya dhati ya kuendelea kuwatumikia, huku wakiahidi kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura ili kumpa ushindi wa kishindo.
Kampeni za ACT-Wazalendo katika jimbo hilo zimekuwa zikihamasishwa kwa nguvu kupitia kauli mbiu za vijana kama #MuhuniHasusiwi, #TheFutureIsPurple na #TheFutureIsACTWazalendo, zikionyesha mshikamano wa chama hicho na kundi kubwa la vijana wanaoamini katika mabadiliko ya kweli.
Kwa ujumla, hali ya kisiasa Pangawe inaonyesha kuimarika kwa ACT-Wazalendo, huku wafuasi wa chama hicho wakiahidi kusimama imara kuhakikisha kura zao hazipotei na ushindi wa chama chao unapatikana kwa njia ya kidemokrasia na halali.

