‎Na Meleka Kulwa -Dodoma 

‎Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Ernest Sungura, ametoa wito kwa waandishi wa habari na wamiliki wa vyombo vya habari kujiunga na Baraza hilo ili liweze kuwasaidia wanapopata madhila yoyote, akisisitiza kuwa umoja ni nguvu.

‎Sungura amesema kwa umoja huo, MCT itakuwa na nguvu zaidi katika kulinda waandishi na kuimarisha demokrasia, utawala bora na vyombo vya habari huru.

‎Ameyasema hayo Septemba 18, 2025 wakati akifungua mkutano wa majadiliano baina ya MCT, waandishi wa habari, maafisa wa idara na mamlaka za serikali uliofanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Nashera Jijini Dodoma.

‎Aidha, Sungura amebainisha kuwa majadiliano hayo yamekuwa yakisaidia kupunguza hofu ya utendaji kazi baina ya taasisi, kuongeza kuaminiana na kuimarisha ushirikiano. Akizungumza, alisema lengo kubwa la majadiliano hayo ni kuimarisha mahusiano ya kikazi kati ya idara na taasisi mbalimbali na waandishi wa habari kwa kuangazia yale yaliyo mazuri, pamoja na kujadili changamoto zinazojitokeza wakati wa utendaji kazi wa pande hizo mbili.

‎“Tutapitia kama tulivyoona kwenye programu, sheria ya kupata taarifa ambayo ndiyo msingi mkuu. Upande mmoja ni watoa taarifa na upande mwingine ni watafuta taarifa. Sheria hii inatupa mwongozo wa jinsi ya kuratibu utoaji na upatikanaji wa taarifa,” amesema Sungura.

‎Aidha, amesema kuwa ni wakati mzuri wa wadau kujua sheria hiyo na kuielewa, kwani ndiyo msingi wa maafisa habari serikalini na taasisi zingine kama Polisi, TAKUKURU hadi kwenye ngazi za kata. Pia, amebainisha changamoto wanazokutana nazo waandishi wa habari wanapotafuta taarifa kwa maafisa ambao hukataa kuzungumza kwa kisingizio cha kutokuwa wasemaji, huku akisisitiza kuwa sheria inatoa haki ya kupata taarifa na kila mmoja anapaswa kutimiza wajibu wake.

‎Sungura pia amesema kuwa majadiliano hayo yataangazia namna waandishi wa habari wanavyoshiriki katika mchakato wa uchaguzi mkuu, akibainisha kuwepo kwa masuala ya kampeni, migogoro ya kisheria na malalamiko mbalimbali ambayo vyote vinapita mikononi mwa vyombo vya habari.

‎Akizungumzia kinga ya waandishi wa habari, Sungura amesema ulinzi wa kweli kwao ni kusema ukweli. “Jiokoe wewe mwenyewe kutoka kwenye mazingira hatarishi kwa kuusema ukweli, kuandika ukweli na kutangaza ukweli. Huyo ndiye mlinzi wako wa kwanza, ili hata ukienda kaburini useme kinga yangu ya kwanza ilikuwa ukweli,” amesema 

‎Aidha, amesisitiza kuwa moja ya majukumu makuu ya MCT ni kusimamia weledi na maadili ya taaluma ya habari, akibainisha kuwa Baraza hilo lina wanachama zaidi ya 300 wakiwemo vyombo vya habari, taasisi za kihabari na vyuo vya uandishi wa habari. Pia alisema MCT lina jukumu la usuluhishi, ambapo wananchi, taasisi za umma au binafsi wanaweza kuwasilisha malalamiko pale wanapoathiriwa na maudhui ya vyombo vya habari.

‎“Baraza hili ndilo mahali pa kisheria ambapo wananchi, taasisi za umma au binafsi wanaweza kuwasilisha malalamiko pale wanapoathiriwa na maudhui ya vyombo vya habari,” amesema Sungura.

‎Aidha, alieleza kuwa Chama cha Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) kina jukumu kubwa katika ngazi za wilaya na mikoa, ambapo kinaratibu shughuli za klabu za waandishi wa habari nchini kote na kushirikiana na wadau wengine wa habari kwa kupata ushauri na mwongozo.

‎Sungura alisema kuwa kwa miaka yote, viongozi mbalimbali wakiwemo mawaziri wakuu wamewahi kutumia utaratibu wa usuluhishi kupitia Baraza hilo na manufaa yake ni kuondoa vyombo vya habari kwenye mtego wa kufilisika na kufilisiwa.

‎Katika mchango wake, mwandishi wa gazeti la Uhuru, Fred Alfred, alishauri MCT kuongeza wigo wa utoaji wa mafunzo kwa waandishi wa habari ili kuongeza uelewa na kuboresha sekta ya habari nchini.

‎Mkutano huo ulihusisha uwasilishaji wa mada mbili kuu. Mada ya kwanza kuhusu Madhila kwa Waandishi wa Habari na mchango wao katika mchakato wa uchaguzi iliwasilishwa na Saumu Mwalimu, Afisa Programu wa MCT. Mada ya pili kuhusu Sheria ya Haki ya Kupata Taarifa iliwasilishwa na Annastazia Rugaba, Mkurugenzi wa Uchechemuzi kutoka Twaweza.

‎