NA JOHN BUKUKU- BAHI- DODOMA
Mgombea wa nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameendelea na kampeni za Uchaguzi katika Wilaya ya Bahi mkoani Dodoma leo Septemba 9, 2025.
Akihutubia wakazi na wananchi wa Bahi, Dkt. Samia amesema kuwa Serikali imepanga kujenga mabweni maalumu kwa ajili ya wanafunzi wa kike. Hatua hiyo inalenga kuimarisha elimu na kuwasaidia watoto wa kike kutokana na changamoto za kimazingira na baadhi ya mila zinazowakwamisha kielimu.
Aidha, ameeleza kuwa ujenzi wa Chuo cha VETA katika wilaya hiyo umekamilika, na kwa sasa kina jumla ya wanafunzi 156 wanaojifunza fani mbalimbali ikiwemo ujenzi, ufungaji wa vyuma, ubunifu na ushonaji, kompyuta pamoja na ufundi umeme wa majumbani na magari. Pia Serikali ina mpango wa kuongeza fani za kilimo na ufugaji ili vijana wanufaike zaidi na fursa zilizopo, zikiwemo skimu za kilimo zilizokarabatiwa zinazowawezesha wananchi kulima mara mbili kwa mwaka.
Kuhusu sekta ya maji, Dkt. Samia amesema miradi ya uchimbaji visima imewezesha vijiji 56 kati ya 59 kupata huduma ya maji safi na salama, huku changamoto kubwa ikibaki katika maeneo ya Mpamantwa. Alisisitiza kuwa mradi mkubwa wa maji kutoka Ziwa Viktoria hadi Dodoma utawanufaisha pia wananchi wa Bahi kwa matumizi ya nyumbani na kilimo.
Aidha, ameeleza kuwa ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) awamu ya pili na ya tatu utahusisha kituo pamoja na bandari kavu katika Bahi, hatua itakayovutia uwekezaji na kuongeza ajira kwa vijana. Kuhusu fidia kwa wananchi waliopisha miradi hiyo, Serikali imeeleza kuwa uhakiki unaendelea na malipo yatatolewa baada ya kukamilika.
Katika sekta ya barabara, amesema kuwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita madaraja tisa na barabara za changarawe zenye urefu wa kilomita 152 zimejengwa, hivyo kurahisisha usafiri wakati wote wa mwaka. Hata hivyo, bado kuna changamoto ya barabara ya Mzogole–Nholi–Ipagala yenye urefu wa kilomita 19 inayohitaji madaraja manne, barabara ya Mtazamo yenye kilomita 12 inayohitaji daraja kubwa kwa ajili ya wakulima wa mpunga, pamoja na barabara ya Chungu–Bahi Sokoni yenye kilomita 6 itakayojengwa kwa awamu mbili, ikianzia na daraja la Mto Koga ambalo limekuwa kero kubwa wakati wa masika.
Dkt. Samia pia ameeleza kuwa Serikali inaendelea na ukarabati wa skimu za umwagiliaji maji kwenye maeneo mbalimbali kwa lengo la kuwajengea vijana uwezo wa kujiajiri kupitia mashamba makubwa ya kilimo.
Vilevile, amewataka wananchi wa Bahi kujitokeza kwa wingi Oktoba 29 kushiriki kupiga kura, akisisitiza kuwa kila aliyeandikishwa anapaswa kushiriki katika zoezi hilo. Aliwaomba pia viongozi wa matawi na mashina kuhakikisha wananchi wote wanashiriki kikamilifu ili kuimarisha utekelezaji wa ahadi zilizotolewa.

