NA JOHN BUKUKU- MANYONI

“Kitajengwa pia kituo cha kuongeza masafa ya FM Manyoni.”

Mgombea urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan, ameahidi kuboresha usikivu wa Radio ya Taifa (TBC) mkoani Singida, ambapo kitajengwa kituo cha kuongeza masafa ya FM katika wilaya ya Manyoni.

Amesema kuwa, Singida kama mkoa umekuwa na changamoto ya usikivu hafifu wa TBC, na kwamba tatizo hilo linashughulikiwa kupitia mradi wa uboreshaji wa usikivu wa TBC unaosimamiwa na Mfuko wa Mawasiliano. Amesisitiza kuwa kituo cha kurushia matangazo ya masafa ya FM kitapewa kipaumbele katika mji wa Itigi ili wananchi wa wilaya hiyo wapate taarifa sahihi za Taifa lao kupitia radio yenye uhakika na ukweli.

“Mkoa wa Singida, hasa eneo la Manyoni, litapitiwa na mradi wa SJR awamu ya tatu unaopita kuelekea Tabora. Mradi huu tunategemea utaufungua mkoa wa Singida na kutengeneza ajira nyingi kwa vijana, kwani kutakuwa na kituo cha mawasiliano na shughuli za kibiashara na uwekezaji zitaimarika,” alisema.

Ameongeza kuwa, maeneo yote ambayo hayajafikiwa na huduma za umeme yataendelea kusambaziwa nishati hiyo, sambamba na upatikanaji wa elimu bora, maji safi na salama, akisisitiza kuwa lengo ni kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma hizo muhimu.

Samia alisema vyama vyote vya siasa vipo katika mzunguko wa kampeni nchi nzima kuomba ridhaa ya wananchi, lakini dhamira ya CCM ni kuhakikisha kinachaguliwa chama kitakachowapa wananchi matumaini ya maendeleo ya baadaye na hatimaye kukabidhiwa jukumu la kuendesha nchi kwa manufaa ya wote.

Akizungumzia sekta ya elimu, alisema wakipata ridhaa watajipanga kujenga chuo cha VETA cha ufundi ndani ya wilaya hiyo, pamoja na kuongeza shule za msingi na sekondari. Alisisitiza kuwa sera ya elimu bila ada itaendelea kama kawaida ili kuhakikisha kila mtoto anapata nafasi ya kusoma.

Aidha, alifafanua kuwa katika ziara yake Manyoni aliweka jiwe la msingi katika eneo la Ulanga, Itigi, ambapo ujenzi wa shule upo katika hatua nzuri kwa asilimia 75.

Kuhusu miundombinu ya barabara, alisema tayari mkandarasi amepatikana kwa ajili ya kutengeneza barabara ya kilometa 31 kutoka Makongorosi, hatua itakayochochea biashara kati ya mikoa ya Singida na Mbeya.

Vilevile, ameongeza kuwa mradi mwingine unaoendelea kusubiri utekelezaji ni ujenzi wa daraja la Sanza, ambapo mkandarasi ameshapatikana na hatua zilizobaki ni kukamilisha upatikanaji wa fedha ili kazi ianze rasmi.