NA JOHN BUKUKU- SINGIDA

Katibu Mkuu mstaafu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Bashiru Ally, amewataka Watanzania kutokuwa na mashaka na Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia CCM, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa sababu ana ujasiri na umakini wa aina yake.

Dkt. Bashiru, ambaye pia ni Mratibu wa Kampeni za chama hicho Kanda ya Kati, alisema hayo leo katika mkutano wa Rais Dkt. Samia wa kunadi sera za CCM, katika Uwanja wa Bombadia mkoani Singida, ikiwa ni kuelekea uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani utakaofanyika Oktoba 29 mwaka huu 

Alisema Rais huyo ni wa kipekee kwani alisimama imara kuivusha nchi katika kipindi kigumu cha mlipuko wa ugonjwa wa Uviko-19, kipindi kilichoambatana na kifo cha Rais wa Awamu ya Tano, Dkt. John Pombe Magufuli.

“Msiwe na mashaka Watanzania wenzangu, huyu kiongozi wetu ana utulivu wa aina yake, ana ujasiri na umakini wa aina yake. Aliyopitia yalihitaji utulivu, yalihitaji umakini, na hayo yote yanatosha kumuongezea nafasi atuongoze,” alisema.

Dkt. Bashiru alimsifu mgombea huyo kuwa ni kiongozi mwenye utulivu na ujasiri wa aina yake katika maamuzi ya uongozi, hivyo yapasa kumchagua tena aiongoze nchi kwa kipindi cha pili cha Awamu ya Sita.

“Maeneo mengine mengi, matukio hayo mawili yakitokea hasa katika nchi zetu ambazo bado zinajijenga huacha maafa makubwa. Mataifa husambaratika, leo taifa letu sio tu lina amani bali pia ni taifa moja. Nilitafiti na nadhani msingi wa sifa hizo zilitokana na uwezo wa Chama Cha Mapinduzi kuwaandaa viongozi,” alisema.

Aliongeza kuwa, “Sio sifa zake peke yake, ni sifa za chama chake kilichomuibua, kilichomlea na kumpa misimamo na yeye akaisimamia. Kwa hiyo huyu sio mgombea bora wa urais tu, bali ni mgombea bora wa urais wa chama bora.”

“Nimekuomba unipe muda kwa sababu pia nimekaa nje ya majukwaa kwa miaka minne, kwa hiyo nimeibukia jukwaani na nguvu nyingi,” alisema huku akishangiliwa na wananchi.

Dkt. Bashiru aliendelea kueleza kuwa kifalsafa na kiitikadi, sera za CCM zinahusu zaidi usawa wa binadamu.

“Usawa wa binadamu ndugu yangu haumaanishi kwamba binadamu wote tutengeneze usawa tuwe na kimo kimoja, hapana. Haimaanishi kuwa na rangi moja wala jinsia moja, hapana. Haiamanishi mapato yanayofanana, hapana. Usawa wa binadamu kwa mujibu wa itikadi na falsafa ya CCM ni kuheshimu utu wa kila binadamu, awe mrefu au mfupi, hata mlemavu, katika suala la heshima ya utu wake yeye ni sawa. Hao wote ni sawa,” alisema.

“Na ndio maana ukisikiliza hiyo habari ya shule, maji, afya—CCM haiwezi kufanya tofauti, kwa sababu itikadi yake na falsafa yake ya usawa wa binadamu inaisukuma kuhakikisha inatoa huduma kwa watu wote ili utu wao usidhalilike. Tajiri na masikini wakikosa maji wote wanadhalilika, mtoto wa masikini na tajiri akikosa elimu wote wanadhalilika. Watoto wa tajiri na masikini wakikosa huduma bora ya afya wote wanadhalilika.

“Kwa hiyo Chama Cha Mapinduzi kinajenga shule, zahanati, vituo vya afya, kinatoa maji na mawasiliano ili kulinda heshima ya utu wa watu wote,” alisema.

Akaongeza: “Kuna hili lingine halisemwi sana. Kwa muda mrefu katika historia ya siasa, nafasi ya mwanamke imekuwa ya pili kana kwamba utu wake ni nusu. Nampongeza sana Harmonize kwa wimbo wake wa Mwanamke ni mtu na nusu. Duniani kote ajenda ya usawa wa kijinsia imekuwa nzito, lakini CCM kwa sababu ya msimamo wa kifalsafa na kiitikadi—usawa wa wanaume na wanawake si suala la hiari, ni suala la lazima.”

Alisisitiza kuwa katika uongozi wa Dkt. Samia, usawa huo umeonekana wazi katika ngazi mbalimbali za uongozi.

“Kitakwimu, angalia maamuzi, sera, miradi na namna utekelezaji wake ulivyoinua hali za kina mama. Hapa Singida tuna mwenyekiti wa chama mwanamke, mkuu wa mkoa mwanamke, RAS mwanamke na katibu wa chama ambaye pia ni mjumbe wa Halmashauri Kuu—mwanamke. Hakuna kilichoharibika kutokana na uongozi wao,” alisema.

Aidha, Dkt. Bashiru alisema katika maeneo mbalimbali ya nchi, wagombea wanawake wameibuka kwa wingi kutokana na ujasiri uliojengewa na uongozi wa Dkt. Samia.

“Lakini pia lipo eneo la elimu. Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, alisema ukitaka kumsaidia mtoto wa masikini mpe elimu. Mimi ni mwalimu wa darasani, nimesoma na kufundisha mpaka ngazi ya shahada ya uzamivu (PhD). Nimeona mabadiliko makubwa katika mfumo mzima wa elimu kutokana na sera ambazo CCM inasimamia, lakini hususan katika kipindi cha uongozi wa Dkt. Samia,” alisema.

“Kwa hiyo ndugu zangu, usawa wa binadamu ndio msingi wa amani, ndio msingi wa umoja wa kitaifa. Tunaposambaza maji nchi nzima bila kujali eneo, kutoa elimu nchi nzima bila kujali eneo—hayo ndiyo misingi ya amani na umoja wa taifa letu,” alisisitiza.

Mwisho wa hotuba yake, Dkt. Bashiru alimwomba radhi Dkt. Samia kwa hisia alizozieleza:

“Mheshimiwa Rais na mgombea wetu, utaniwia radhi, sijawahi kusema jambo hili kwa sababu nimekuwa nikijizuia sana kutokana na hisia zilizotokana na ushuhuda niliouona katika kipindi kile ulipokuwa unakabidhiwa madaraka.

Kwa hiyo Wanasingida hamjakosea kufurika katika mkutano huu kwa bashasha, shangwe na uchangamfu kumlaki na kumuahidi kura nyingi tarehe 29 Oktoba.”