NA JOHN BUKUKU- DODOMA

Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan kesho, anatarajiwa kuanza kampeni zake mkoani Singida Septemba 9, 2025, mara baada ya kukamilisha ziara yake ya kampeni katika Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, iliyohusisha mikoa ya Songwe, Mbeya, Njombe na Iringa.

Katika ziara hiyo, Dkt. Samia alipata mapokezi makubwa ya wananchi na kutumia fursa hiyo kueleza vipaumbele vya Serikali ya Awamu ya Sita katika sekta mbalimbali iwapo atachaguliwa.

Akiwa mkoani Songwe na Mbeya, aliahidi kuimarisha miundombinu ya barabara, kuboresha Reli ya TAZARA  na kujenga bandari Kavu eneo la Katenjele Mpemba mkoani Songwe ili kuongeza kasi ya usafirishaji wa mazao ya kilimo, hususan Kahawa, Parachichi ikiwemo Pareto ambayo yamekuwa nguzo muhimu ya uchumi wa mikoa hiyo.

Aidha, akiwa mkoani Njombe, Dkt. Samia alitangaza mpango kabambe wa wa kujenga uwanja mpya wa ndege utakaowezesha usafirishaji wa bidhaa za kilimo moja kwa moja kwenda masoko ya kimataifa na maghala maalum ya kuhifadhi Parachichi kabla ya kusafirishwa masoko ya nje. Pia aliahidi kuajiri maafisa ugani  kusaidia wakulima wa chai na parachichi ili kuongeza tija ya uzalishaji.

Mkoani Iringa, mgombea huyo alipata baraka za Chifu wa Wahehe, Chifu Abdul Sapi Mkwawa II, jambo lililotafsiriwa kama ishara ya mshikamano wa kijamii na kisiasa. Aidha, aliahidi kuanzisha ujenzi wa soko la kisasa la machinga katika eneo la Stendi ya zamani mjini Iringa na kuboresha huduma za kijamii hususan afya na elimu ikiwemo miundombinu.

Kwa mujibu wa viongozi wa CCM na wananchi, mapokezi makubwa yaliyoshuhudiwa katika mikoa yote minne ni kielelezo cha imani kubwa kwa chama hicho na serikali yake, hali inayotoa matumaini ya ushindi mnono katika uchaguzi ujao.

Kuanza kwa kampeni mkoani Singida kunatarajiwa kuwa na mwendelezo wa ahadi za chama hicho, ambapo Dkt. Samia atakutana na wananchi kwa ajili ya kueleza sera na mikakati ya kuimarisha kilimo cha alizeti, kuongeza thamani ya mafuta ya kula, na kuboresha miundombinu ya barabara, Afya na maji.

Kwa mujibu wa ratiba ya chama hicho, Singida  inatarajiwa kuwa kitovu cha kampeni zinazofuata kwa kufanyika mkutano mkubwa kama ilivyofanyika katika mikoa mingine, zikijikita katika kuhamasisha wananchi kushiriki uchaguzi na kuunga mkono CCM kwa kile kinachoelezwa kuwa ni utekelezaji wa vitendo wa Ilani ya Uchaguzi