MGOMBEA mwenza wa Kiti cha Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi akiwahutubia Wananchi wa Jimbo la Kwela katika Uwanja wa Laela A,Sumbawanga Vijijini katika mkutano mdogo wa hadhara wa Kampeni leo Jumatatu Septemba 8,2025.
……………
Na Neema Mtuka, Sumbawanga Vijijini
Mgombea mwenza wa urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, ameahidi wananchi wa Rukwa kuboresha barabara za Bonde la Ziwa Rukwa, kujenga stendi mpya ya Laela, kupanua huduma za maji safi na salama pamoja na kuanzisha viwanda vya kusindika mazao ya chakula na maziwa ili kukuza uchumi wa wakulima.
Akihutubia wananchi wa Laela leo Septemba 8, Dkt. Nchimbi alisema changamoto zote za barabara zitapatiwa ufumbuzi mara baada ya CCM kupewa ridhaa ya kuunda serikali kwa kipindi kingine cha miaka mitano. Aliongeza kuwa serikali itahakikisha ndani ya siku 100 za kwanza, inatekeleza vipaumbele muhimu vikiwemo upatikanaji wa bima ya afya kwa wote, kwa kuzingatia zaidi wajawazito, watoto, wazee na watu wanaoishi na ulemavu.
“Serikali ya CCM katika kipindi cha miaka mitano iliyopita imepiga hatua kubwa katika sekta mbalimbali ikiwemo elimu, ambapo ajira za walimu zimeongezeka kutoka 1,485 hadi 1,960. Vilevile shule za msingi zimeongezeka kutoka 104 hadi 117 na shule za sekondari kutoka 16 hadi 25, hali iliyopanua fursa za kielimu kwa vijana wetu,” alisema Dkt. Nchimbi.
Awali, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Rukwa, Hajat Ashraf Maufi, alimwomba mgombea mwenza huyo kuhakikisha maboresho ya barabara ya Bonde la Ziwa Rukwa yanafanyika haraka ili kuondoa changamoto za usafiri na usafirishaji.
“Nakuomba Mheshimiwa Nchimbi, wewe na mgombea wa urais mkipata ridhaa, ndani ya siku 100 natamani kuona utekelezaji wa ilani yetu,” alisema Maufi.
Katika mkutano huo, Mchungaji Peter Msigwa, ambaye aliwahi kuwa mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), alieleza namna Serikali ya CCM ilivyotekeleza ilani yake ya uchaguzi kwa kipindi cha 2020 hadi 2025 kupitia miradi mikubwa ya kitaifa.
Alisema miradi hiyo inajumuisha ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR, miradi ya maji katika miji 28 na ujenzi wa shule mpya za sekondari, hatua ambazo zimepanua fursa za elimu na huduma za kijamii nchini. 

