Mgombea wa Kiti cha Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Samia Suluhu Hassan akizungumza na wananchi wa Kata ya Kalenga wilaya ya Iringa Vijijini kwa Chifu Mkwawa waliojitokeza kwa wingi kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika leo Septemba 6,2025 mkoani Iringa.

…………

NA JOHN BUKUKU- KALENGA

Mgombea wa Kiti cha Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Samia Suluhu Hassan, amesema amefurahi kupata baraka za Chifu Abdul Sapi Mkwawa,Mfwimi wa II wa kabila la Wahehe, alipokuwa akiendelea na kampeni zake katika eneo la Kalenga, mkoani Iringa.

Ikumbukwe Watanzania wanatarajia kufanya Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani tarehe 29 Oktoba mwaka huu.

Akizungumza baada ya kukutana na Chifu Mkwawa, Dk. Samia alisema: “Nimefurahi kupata baraka za kichifu nikiwa hapa Kalenga. Mimi naitwa Chifu Hangaya, ni Chifu Mkuu hapa Tanzania, lakini nilikuwa sijawahi kufika hapa kupata baraka za Chifu Mkwawa. Leo nimefurahi sana.

Nimefarijika pia kuonana na ndugu zangu Wahehe wa Mkwawa wanaosifika kwa ujasiri na ari ya kupambana. Sasa mapambano yetu ni ya kujenga Taifa lenye uchumi jumuishi, linalojitegemea kiuchumi na lenye ustawi. Ndio sababu nimekuja hapa kwenu, wanaMkwawa, kuwaomba kura zenu ili tuingie pamoja kwenye mapambano ya kuijenga Tanzania tunayoitaka.

“Nashukuru kwa mapokezi makubwa, upendo na ukarimu mlionionesha. Asanteni sana,”alisema Rais Samia.

Kwa upande wake, Chifu Abdul Sapi Mkwawa II alimshukuru Dk. Samia kwa mchango wake mkubwa katika maendeleo ya wananchi wa Tanzania, hususan wanaIringa na wanaKalenga.

“Kwa kuelewa harakati zako nzuri Mheshimiwa Rais, tunakushukuru kwa yote unayotufanyia sisi Wahehe, wanaIringa na wanaKalenga. Nimeona ni muhimu kutoa baraka zetu kutoka kwa mababu ili zikulinde na kukuongoza, ukapate miaka mingine mitano ya kuendelea kutuongoza.

Eneo hili la Kalenga limekuwa na historia kubwa sana katika maisha yangu na maisha ya wanakijiji. Wewe ni Rais wa pili kufika hapa; mara ya kwanza alikuwa Mheshimiwa Jakaya Kikwete, aliyefika kwa ajili ya mazishi. Lakini wewe umefika kwa ajili ya kuomba kura na kutupa matumaini mapya.

Tunajua mengi yamefanyika katika mkoa wetu; barabara zimeboreshwa na kuwezesha masoko kufanya kazi vizuri, tumepata hospitali nzuri, na mashule yameongezwa ili vijana wetu wapate elimu. Kwa yote haya tunaamini mababu zetu wanaona. Tunaomba waendelee kukulinda na kukupa amani katika uongozi wako, alisema Chifu Mkwawa.