NA JOHN BUKUKU, MBALIZI

Wananchi wa Wilaya ya Mbeya Vijijini, hususan mji mdogo wa Mbalizi, wameeleza kuwa wana shauku kubwa ya kumpokea mgombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye anatarajiwa kufanya mkutano mkubwa wa hadhara Septemba 4 mwaka huu.

Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM Wilaya ya Mbeya Vijijini, ambaye pia ni mwanakamati wa hamasa, Festo Ambilike, amesema ujio wa Dkt. Samia katika eneo hilo ni surprise kubwa kwa wananchi, kwani mara ya mwisho mkutano wa urais kufanyika katika wilaya hiyo ilikuwa miaka ya 1990.

“Kwa historia ya wilaya yetu, hatujawahi kuwa na mikutano ya mara kwa mara inayofanyika kumpokea Rais. Safari hii mama Samia ametupa surprise kubwa kwa kuamua kutia mguu wake kwenye ardhi ya Mbalizi. Nasi kama wananchi tumejipanga kumlipa kwa ‘Kutiki’ pia kwa maandalizi makubwa na mapokezi yenye heshima,” amesema Festo.

Amesema wananchi wa Mbeya Vijijini wanatambua jitihada kubwa zilizotekelezwa na Rais Samia katika sekta mbalimbali ikiwemo maji, afya na maboresho ya barabara, jambo linalowapa hamasa ya pekee ya kujitokeza kwa wingi.

“Hamasa ni kubwa sana, tumefikia asilimia 90 ya maandalizi. Tunatarajia zaidi ya watu elfu 20 kuhudhuria, na vijana zaidi ya elfu moja wamepanga kufanya matembezi maalum ya shamrashamra kumkaribisha mama Samia,” amesema Festo.

Amefafanua kuwa mkutano huo utafanyika katika viwanja vya Mlima Reli, Mbalizi, ambapo wananchi kwa wingi wanatarajiwa kujitokeza kumsikiliza Dkt. Samia na kushuhudia ahadi zake kwa wananchi.

Aidha, amesema ujio huo umekuwa wa kihistoria kwa kuwa umetimiza kiu ya muda mrefu ya wananchi kutaka kuona mikutano ya urais ikifanyika kwenye wilaya yao.

“Wananchi wanamshukuru sana Rais Samia kwa kutupendelea kuchagua Mbalizi. Wanapanga kumlipia surprise kwa mapokezi makubwa, kwani kwa miaka mingi walikuwa na kiu ya kuona mkutano wa aina hii. Kwa hakika siku ya Septemba 4 itakuwa ya kihistoria,” amesema Festo.

Naye Prisca Michael mama mjasiriamali mkazi wa kijiji cha Ifuekenya amesema zamani ilikiwa unabeba mimba unatoka kule kijijini mpaka ufike hospitali mjini, pengine unajifungulia njiani au unepoteza maisha. Lakini sasa hivi hali imebadilika. Mfano, hapo kijiji cha Ifyekenya tayari kuna zahanati, Chang’ombe ipo kubwa zaidi na Mbuyuni kuna kituo cha afya kikubwa zaidi. Hivyo ni vituo vikubwa ambavyo zamani havikuwepo na vimejengwa hivi karibuni.

“Zamani tulikuwa tunategemea hospitali ya Ifisi pekee, lakini sasa hivi huduma ya afya ya mama na mtoto imesogezwa mpaka vijijini na hali ya afya imeboreshwa sana. Tunamshukuru Rais Samia kwa kutuletea huduma hizi, kwani kwa sasa hali ni nzuri na hatuhangaiki kama zamani ambapo wajawazito walikuwa wanapata tabu sana kujifungua na wengine kupoteza maisha, ” Amesema Prisca. 

Ameongeza kuwa ujio wa Mgombea Urais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni furaha kwetu kwamba mama anakuja Mbeya kwenye kampeni. Kwa kutuletea huduma hizi tayari ameshafanya yake, sisi kilichobaki ni kumlipa tiki tu Oktoba 29, 2025.

“Mimi ni mjasiriamali, nauza mchele. Natamani nimuone ili anipe hata mtaji niongezee kwenye biashara yangu, nami niwe mfanyabiashara mkubwa,” amesema Bi Prisca Michael, mzaliwa wa kijiji cha Ifyekenywa.

Naye Aloyce Kaniki, Afisa Usafirishaji katika lango kuu la Stendi ya Mbalizi, amesema amesikia ahadi za Mgombea Urais kwa tiketi ya CCM, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhusu Bima ya Afya kwa Wote. Amesema kuwa hilo ni jambo zuri na linatia moyo.

Kwa upande wake kama Afisa Usafirishaji, amesema bima ni muhimu sana, kwani kwa sasa waendesha bodaboda wanakabiliana na changamoto nyingi ikiwemo ajali zinazoweza kusababisha majeraha na ulemavu. Ameeleza kuwa kuanza kwa utekelezaji wa mpango wa Bima ya Afya kwa Wote ni ahueni kubwa, kwa sababu itawasaidia wanapokumbana na changamoto za kuumwa au kujeruhiwa katika kazi zao za kila siku.

Ameongeza kuwa nia ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni njema sana, lakini ugumu unakuja kwenye utekelezaji. “Wakati mwingine unakuta wagonjwa wawili wanapata matatizo, lakini mnapokwenda hospitalini yule anayelipa pesa taslimu anapewa kipaumbele kuliko mwenye bima. Tunaiomba Serikali izingatie changamoto hii ili mpango huu uwe na manufaa kwa wote,” amesema Kaniki.