NA JOHN BUKUKU, KONDOA- DODOMA
Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, John Mongela, amemuelezea mgombea urais kupitia CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kama Kiongozi aliyeibua matumaini mapya kwa Watanzania kutokana na dira na kazi kubwa alizofanya katika uongozi wake.
Akizungumza kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika Kondoa, mkoani Dodoma, Agosti 31, 2025, Mongela alisema imani ya wananchi kwa Dkt. Samia inazidi kuongezeka kila siku, jambo linalodhihirisha matumaini ya taifa kuelekea kwenye kesho iliyo bora.
Mongela alisema wananchi si wanachama wa CCM pekee ambao waliojitokeza kumpokea mgombea huyo, bali hata wale wasiokuwa wanachama wameacha shughuli zao za kila siku na kuungana naye kwa shangwe na matumaini.
“Kule Uswahilini tunasema wali wa kushiba unaonekana jinsi ulivyojaa kwenye sinia. Maana yake hawa watu unaweza kujiuliza wanapata nini? Wamepata matumaini kwa mgombea wetu ambaye ameunganishwa na Taifa,” alisema Mongela.
Aidha, Mongela alisisitiza kuwa Watanzania wanamwona Dkt. Samia kama kiongozi mwenye majibu ya matarajio yao katika sekta mbalimbali za kijamii na kiuchumi. “Mheshimiwa Rais, kuna matumaini makubwa sana kwenye nchi yetu na taifa zima juu yako.
Kama Chama Cha Mapinduzi umetuletea faraja kubwa. Tunakuombea Mwenyezi Mungu azidi kukulinda, kukubariki na kukusimamia ili nchi hii tuione kesho iliyo njema,” alisema.
Kwa mujibu wa Mongela, mwamko wa wananchi unaoonekana katika mikutano ya kampeni ni uthibitisho kwamba Watanzania wanaamini katika uongozi wa Dkt. Samia na wanauona mwelekeo wa maendeleo na mshikamo wa kitaifa.

