Mwamvua Mwinyi – Pwani
Agosti 26, 2025
Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Pwani kimesema hakitishwi na mihemko ya baadhi ya wanachama wanaokihama chama hicho kutokana na kukosa kuteuliwa katika nafasi mbalimbali, kikieleza kuwa uamuzi wa mtu kuondoka ni haki yake ya hiari.
Aidha, chama hicho kimeonya vikali wanachama wa kivuli wanaoshabikia au kushabihiana na wanaoihama CCM, kikisema kuwa endapo watabainika, hatua kali za kinidhamu zitachukuliwa dhidi yao.
Akizungumza na waandishi wa habari, ofisini kwake ,mjini Kibaha kuelekea uzinduzi wa kampeni za Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Agosti 28, 2025, Katibu wa Siasa, Uenezi na Mafunzo wa CCM Mkoa wa Pwani, David Mramba, alieleza chama hakijamtuma mwanachama yeyote kukihama chama.
“Kuna baadhi ya wanachama waliokosa uteuzi katika vikao vya maamuzi vya wilaya, mkoa na taifa, na wameamua kuhama chama kwenda vyama pinzani ambako wanapewa nafasi za uongozi, Huu ni uamuzi wa mtu binafsi, na CCM haiwezi kuzuiwa na matakwa ya mtu mmoja,” alisema Mramba.
Aliongeza kuwa CCM ni chama madhubuti na kinachoendelea kuimarika, kikiwa ni chama cha tisa kwa idadi kubwa ya wanachama duniani.
“CCM ni chama dume, Kinaongoza kwa idadi ya wanachama Tanzania na ni cha tisa duniani kwa kuwa na wanachama wengi,Tuna uhakika na nguvu yetu,” alisisitiza.
Mramba alisisitiza umuhimu wa wanachama kuwa na ukomavu wa kisiasa, kushikamana na kuendeleza umoja ndani ya chama ili kuhakikisha ushindi wa kishindo katika uchaguzi wa Oktoba 29, 2025.
Katika hatua nyingine, aliwataka Wabunge na Madiwani walioteuliwa kutumia majukwaa ya kampeni kusisitiza mafanikio makubwa yaliyopatikana kupitia Ilani ya CCM 2020–2025 na kuwaeleza wananchi dhamira ya chama kuwaletea maendeleo endelevu.
Pia, Mramba aliwaomba wananchi na wana-CCM wote kujitokeza kwa wingi katika uzinduzi wa kampeni kitaifa utakaofanyika Agosti 28, 2025, katika Viwanja vya Tanganyika Packers, Kawe – Dar es Salaam.
“Tujitokeze kwa wingi kuonesha mshikamano na nguvu ya chama chetu,” alihitimisha.
