Na Silivia Amandius.
Missenyi, Kagera.
Zaidi ya shilingi bilioni 135, sawa na asilimia 93.8, zimetumika kuendesha miradi mikubwa ya maendeleo katika Jimbo la Missenyi, mkoani Kagera, kwa kipindi cha miaka mitano.
Fedha hizo zimetolewa na Serikali Kuu kwa kushirikiana na Mbunge wa Jimbo hilo, Mhe. Florent Kyombo, na zimechangia kwa kiasi kikubwa kuboresha huduma muhimu kwa wananchi, hususani katika sekta za afya, elimu, maji safi, na miundombinu ya barabara.
Aidha, kiasi cha bilioni 8.934 sawa na asilimia 6.2, kimetumika katika miradi mingine midogo na kusaidia kuondoa changamoto zilizokuwa zikiwakabili wananchi wa Missenyi kwa muda mrefu.
Katika ziara aliyoifanya hivi karibuni kwenye kata za Bwanjai, Kashenye, na Kanyigo, Mhe. Kyombo alikutana na wananchi kwa lengo la kueleza utekelezaji wa miradi hiyo kupitia Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kuendelea kusikiliza changamoto mpya zinazowakabili.
Akizungumza katika mikutano hiyo, Mhe. Kyombo alieleza kuwa mafanikio hayo ni ushahidi wa dhamira ya kweli ya kuwahudumia wananchi, akisisitiza kuwa uongozi bora haupimwi kwa mali, bali kwa kiwango cha utu, uaminifu na uadilifu wa kiongozi.
“Tumeshuhudia viongozi wengi wenye uwezo wa kifedha lakini hawana nia ya kweli ya kuwatumikia wananchi. Naomba tuendelee kuchagua viongozi wenye hofu ya Mungu, walio tayari kusikiliza na kushughulikia changamoto zenu kwa moyo wa dhati,” alisema Mhe. Kyombo.
Wananchi waliokutana naye walieleza kuridhishwa na utekelezaji wa miradi hiyo, wakisema kuwa maendeleo yameonekana kwa vitendo, hususan katika huduma za maji na afya.
Ziara hii ni sehemu ya juhudi za Mhe. Kyombo kuimarisha ushirikiano na wananchi, huku akiendelea kujiandaa kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka ujao.

