Na Mwandishi Wetu,
Geneva, Uswizi – Juni 5, 2025
Katika harakati za kimataifa za kukabiliana na athari za majanga, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Duniani (WMO), Celeste Saulo, ameahidi kuisaidia Tanzania kuimarisha mifumo ya tahadhari ya mapema kwa lengo la kuongeza uwezo wa kuchukua hatua za haraka kabla na wakati wa maafa.
Akizungumza mjini Geneva, Uswizi, katika kikao cha pembezoni mwa Jukwaa la Nane la Dunia la Kupunguza Madhara ya Maafa, Saulo alieleza dhamira ya WMO kushirikiana na Tanzania kwa karibu zaidi. Katika mazungumzo yake na Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, na Uratibu, Dkt. Jim Yonazi, Saulo alieleza kuwa taasisi yake iko tayari kusaidia maeneo mbalimbali ya kiufundi na mafunzo ili kuhakikisha mfumo wa tahadhari za mapema unakuwa imara zaidi nchini.
“Tuna nia ya dhati ya kushirikiana na Tanzania katika kuongeza uwezo wa kitaalamu, kuimarisha matumizi ya teknolojia ya kisasa ya utabiri wa hali ya hewa, na kuendeleza elimu ya matumizi sahihi ya taarifa za hali ya hewa katika kupunguza madhara ya majanga,” alisema Saulo.
Akiipongeza Tanzania kwa juhudi zake katika menejimenti ya maafa, Saulo alisema nchi hiyo imekuwa mfano wa kuigwa katika ukanda huu kwa kuanzisha mifumo madhubuti ya tahadhari ya mapema na kuwa na taasisi zenye uwezo wa kutoa taarifa za tahadhari kwa wakati.
Kwa upande wake, Dkt. Yonazi alielezea msimamo wa Serikali ya Tanzania wa kuendeleza ushirikiano huo na taasisi za kimataifa kama WMO, akisisitiza kuwa ni sehemu ya mkakati wa kuifanya jamii kuwa stahimilivu dhidi ya majanga mbalimbali yanayoweza kujitokeza.
“Tunaendelea kujenga mifumo imara inayozingatia sheria, kanuni, na taratibu zilizopo ili kuhakikisha taifa letu linakuwa salama. Tunaona mafanikio makubwa, yakiwemo ya uanzishwaji wa Kituo cha Taifa cha Ufuatiliaji wa Mwenendo wa Majanga na Tahadhari ya Mapema, ambacho kimekuwa chombo muhimu katika kutoa taarifa kwa haraka,” alibainisha Dkt. Yonazi.
Mazungumzo hayo yameweka mkazo kwenye haja ya kuwa na maendeleo jumuishi yanayojumuisha wadau wote wa ndani na nje ya nchi, ili kuongeza nguvu katika mapambano dhidi ya maafa, na kuwezesha jamii kunufaika na hatua zinazochukuliwa mapema.
Kwa pamoja, viongozi hao wameahidi kuweka mikakati madhubuti ya kuendeleza ushirikiano huu ili kuhakikisha taarifa za hali ya hewa zinawafikia wananchi kwa wakati, na hatua za kuzuia madhara ya majanga zinachukuliwa mapema kabla ya athari kutokea.

