Na Silivia Amandius.
Missenyi, Kagera.
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoani Kagera imetoa elimu ya mlipakodi kwa wavuvi katika mwalo wa Marehe, uliopo kijiji cha Marehe, kata ya Rubafu, wilayani Misenyi, mkoani Kagera.
Akizungumza na waandishi wa habari Mei 29, 2025, wakati wa zoezi hilo, Afisa Elimu na Mawasiliano wa TRA Kagera, Bw. Rwekaza Rwegoshora, alisema kuwa lengo ni kusogeza huduma karibu na wananchi ili kuwaondolea adha ya kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za usajili wa biashara na ulipaji kodi katika Makao Makuu ya TRA yaliyopo Bukoba Mjini.
Bw. Rwegoshora alieleza kuwa kampeni ya utoaji elimu ya kodi kwa wananchi inaendelea katika maeneo mbalimbali yenye mialo mkoani humo, akiwahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kupata elimu hiyo na kusajili biashara zao mahali walipo.
“Utoaji wa elimu hii umelenga kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu umuhimu wa ulipaji kodi na kusajili biashara zao kisheria. Hii itasaidia kuongeza wigo wa walipakodi na mapato ya serikali,” alisema Rwegoshora.
Aidha, alikemea tabia ya baadhi ya wananchi kuingiza bidhaa nchini bila kufuata taratibu za forodha, akisisitiza kuwa ni muhimu kuzingatia sheria ili serikali ipate mapato ya kugharimia maendeleo ya miundombinu na huduma nyingine muhimu kwa wananchi.
Mmoja wa wavuvi walionufaika na elimu hiyo, Bw. Paulo Nshekanabo Ribent, alisema elimu aliyopata imemwezesha kusajili biashara yake rasmi kwa mara ya kwanza, jambo ambalo hapo awali halikuwa rahisi kutokana na ukosefu wa uelewa.
“Nawashauri wananchi wenzangu waitumie elimu hii vizuri kwa kusajili biashara zao na kulipa kodi kwa wakati. Nashukuru TRA kwa kutuletea huduma hii karibu,” alisema Nshekanabo.
Zoezi hili ni sehemu ya juhudi za TRA kuimarisha ukusanyaji wa mapato kwa kusogeza huduma kwa wananchi walioko maeneo ya pembezoni.