Nyasa, Ruvuma – Mradi wa Tanzania Project umefanikisha ujenzi wa shule mpya ya Sekondari Lovund na kuikabidhi rasmi kwa Serikali katika hafla iliyofanyika tarehe 12 Machi 2025 kwenye viwanja vya shule hiyo. Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali na wadau wa elimu, huku mgeni rasmi akiwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Ahmed Abbas Ahmed, aliyewakilishwa na Mkuu wa Wilaya ya Nyasa, Mhe. Peres Magiri.
Katika hotuba yake, Mhe. Magiri alisisitiza umuhimu wa mradi huo katika kuboresha elimu wilayani Nyasa. “Ujenzi wa shule hii umekuwa mkombozi kwa wananchi ambao hapo awali walilazimika kutembea zaidi ya kilometa saba kufuata elimu ya sekondari. Sasa wanafunzi watasoma katika mazingira mazuri yenye miundombinu ya kisasa inayowahamasisha katika masomo yao,” alisema.
Aliwataka walimu, wazazi, na wanafunzi kutunza majengo hayo ili kuhakikisha elimu bora inaendelea kutolewa kwa kizazi cha sasa na vijavyo. Pia, alimpongeza Mratibu wa Mradi wa Tanzania Project, Mwl. Dennis Katumbi, kwa usimamizi mzuri wa mradi huo.
Akiwasilisha taarifa ya mradi huo, Mwl. Dennis Katumbi alisema kuwa Tanzania Project unatarajiwa kugharimu Shilingi Bilioni 1.2 hadi kukamilika kwake. Hadi sasa, Shilingi Milioni 998 zimetumika, huku asilimia 87 ya miundombinu ikiwa imekamilika. Serikali kuu pia imetoa Shilingi Milioni 20 kusaidia kukamilisha bweni la wasichana, ambalo liko katika hatua za mwisho za ujenzi.
Miundombinu iliyojengwa inajumuisha: Vyumba 8 vya madarasa, Nyumba 3 za walimu (Three in One kila moja), Nyumba ya Mkuu wa Shule, Jengo la Utawala, Maabara 3, Matundu ya vyoo 17 kwa wanafunzi na 2 kwa watumishi, Maktaba (inayoendelea kujengwa), Bwalo la chakula na jiko, Uzio wa shule (unaendelea kujengwa) na Tanki la maji la lita 5,000.
Kwa mujibu wa Katumbi, mradi huo umepangwa kutekelezwa katika awamu nne, ambapo awamu tatu tayari zimekamilika. Awamu ya nne na ya mwisho, inayojumuisha ujenzi wa maktaba, nyumba moja ya walimu, kichomea taka, na uzio wa shule, inatarajiwa kukamilika ifikapo 31 Mei 2025.
Mbunge wa Jimbo la Nyasa, Mhandisi Stella Manyanya, aliipongeza Tanzania Project kwa mchango wake katika elimu na kusisitiza kuwa uwekezaji katika miundombinu ya shule ni hatua muhimu katika kuleta maendeleo wilayani Nyasa. “Natoa wito kwa wazazi kuhakikisha watoto wao wanatumia fursa hii kwa manufaa yao ya kielimu,” alisema.
Mkurugenzi wa Tanzania Project, Hanne, alitoa shukrani kwa wafadhili wa mradi huo kutoka Norway, wakiwemo Familia ya INO na Henca Foundation, kwa mchango wao mkubwa katika kufanikisha ujenzi wa shule hiyo. “Elimu ni ufunguo wa maisha, tunamatumaini kuwa shule hii itachangia kuwasaidia wanafunzi kupata mafanikio katika maisha yao,” alisema.
Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa alipokea hati ya makabidhiano ya shule hiyo kwa niaba ya Serikali na kuahidi kuwa majengo hayo yatatunzwa ili kuhakikisha utoaji wa elimu bora kwa wanafunzi wa sasa na vizazi vijavyo.
Mwakilishi wa Ubalozi wa Norway alisisitiza kuwa ushirikiano kati ya Tanzania na Norway utaendelea kuimarika, huku akipongeza ubora wa shule hiyo na mchango wake kwa jamii ya Nyasa.
Kwa ujumla, Mradi wa Tanzania Project umeonyesha dhamira ya kusaidia maendeleo ya elimu nchini kwa kujenga shule ya kisasa wilayani Nyasa. Kukamilika kwa shule hii kutapunguza changamoto ya umbali kwa wanafunzi, hivyo kuwapa fursa nzuri ya kupata elimu bora katika mazingira salama na rafiki kwa ujifunzaji.