Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini na Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde,akikata utepe kuashiria ugawaji wa kompyuta na printer kwa shule 50 za sekondari zilizopo Jijini Dodoma, sambamba na kuzindua maabara ya kisasa ya chumba cha kompyuta,hafla iliyofanyika leo Machi 10, 2025, katika Shule ya Sekondari Viwandani.
Na Alex Sonna-DODOMA
Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini na Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, amesema kuwa katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kumekuwa na mabadiliko makubwa katika sekta ya elimu nchini, ikiwemo ujenzi wa vyuo vya VETA, shule za msingi na sekondari, hatua ambayo imeondoa adha kwa wananchi kuchangishwa fedha kwa ajili ya ujenzi wa shule.
Mhe. Mavunde ameyasema hayo leo Machi 10, 2025, katika Shule ya Sekondari Viwandani alipokuwa akikabidhi kompyuta na printer kwa shule 50 za sekondari zilizopo Jijini Dodoma, sambamba na kuzindua maabara ya kisasa ya chumba cha kompyuta na kugawa kompyuta kwa ofisi zote za kata 41 zilizopo ndani ya Jiji la Dodoma.
Waziri Mavunde amebainisha kuwa ongezeko la shule limeleta matokeo chanya katika kuboresha elimu jijini Dodoma.
“Tumeanza kuona matunda ya kazi iliyofanyika, Shule za msingi na sekondari zimeongezeka sana, Nyie ni mashahidi—shule za msingi zilikuwa 96, lakini leo tuna shule 107, ndani ya miaka miwili pekee, shule mpya 11 zimejengwa,” amesema Mhe. Mavunde.
Waziri Mavunde ameeleza kuwa kompyuta hizo zitakuwa na nyaraka muhimu kwa wanafunzi, ikiwa ni pamoja na mitihani ya taifa iliyopita ya kidato cha pili, kidato cha nne, na kidato cha sita kuanzia mwaka 1988 hadi 2024.
“Kompyuta hizi zitakuwa na mitihani ya taifa iliyopita ya kidato cha pili, kidato cha nne, na kidato cha sita kuanzia mwaka 1988 mpaka mwaka 2024. Hii itasaidia wanafunzi kujifunza kwa urahisi na kwa ufanisi zaidi,” amefafanua Mhe. Mavunde.
Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Viwandani, Mwl. Ester Simchimba, amemshukuru Mhe. Mavunde kwa mchango wake mkubwa katika kusimamia taaluma na kuboresha miundombinu ya elimu jijini Dodoma.
“Mheshimiwa Mavunde amekuwa mdau mkubwa wa elimu hapa Dodoma. Amehakikisha mazingira ya kujifunzia yanaboreshwa na taaluma inaendelea kukua,” amesema Bi. Ester.
Ameongeza kuwa, kwa jitihada za serikali ya awamu ya sita pamoja na mchango wa Mbunge Mavunde, azma ya elimu bure yenye mazingira safi na rafiki kwa wanafunzi imefanikiwa kwa kiwango kikubwa jijini Dodoma.