Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi wa Bodi ya Mfuko wa Barabara (RBF) na Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Mfuko huo,Mhandisi Rashid Kalimbaga ( katikati ),leo akiwa na wajumbe wa baraza hilo,katika picha ya pamoja,baada ya kikao kujadili na kupitisha bajeti ya RBF ya mwaka wa fedha wa 2025/26, mkoani Morogoro.
Baadhi wa Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Bodi ya Mfuko wa Barabara (RBF),wakiimba wimbo wa Solidality Forever wakiwa wameshikana mikono katika kikao kujadili na kupitisha bajeti ya mfuko huo kwa mwaka wa fedha wa 2025/26,leo mkoani Morogoro.
Picha na Baltazar Mashaka.
Na BALTAZAR MASHAKA,MOROGORO
WAJUMBE wa Baraza la Wafanyakazi wa Bodi ya Mfuko wa Barabara (RBF) wamekutana mkoani Morogoro,kujadili na kupitisha bajeti ya bodi ya mfuko huo kwa mwaka wa fedha 2025/26.
Mwenyekiti wa Baraza hilo na Mtendaji Mkuu wa RBF,Mhandisi Rashid Kalimbaga,akizungumza na waandishi wa habari mkoani humo,amesema kuwa bajeti hiyo imezingatia majukumu makubwa ya bodi na inatoa kipaumbele katika kuainisha vyanzo vipya vya mapato ya Mfuko wa Barabara.
Pia,ufuatiliaji wa matumizi ya fedha za matengenezo ya barabara zinazopelekwa kwa Wakala za Barabara nchini (TANROADS)na Wakala wa Barabara za Mijini Vijijini(TARURA) na kuhakikisha fedha zinazokusanywa za matengenezo ya barabara zinapelekwa kwa wakati kwa wakala za barabara,kuwezesha mtandao wa barabara nchini wenye jumla ya kilomita 188,000 kupitika majira yote ya mwaka.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Mipango na Mapato wa RBF,Godlove Stephen,amesema bajeti ya mwaka wa fedha 2025/26,imejikita katika kufanya tafiti mbali mbali zitakazowezesha upatikanaji wa vyanzo vipya vya mapato ya Mfuko wa Barabara ili kuongeza uwezo wa mfuko kugharamia mategenezo ya barabara nchini.
Pia,kuimarisha usimamizi wa makusanyo yatokanayo na hifadhi za barabara na kuboresha matumizi yake,kuongeza fursa za ajira na kipato kwa Watanzania watakaotumia hifadhi za barabara kufanya biashara mbalimbali ili kujikwamua kiuchumi.
Naye Rehema Lungo,kwa niaba ya wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Bodi ya Mfuko wa Barabara amesema bajeti hiyo ya mfuko imepita bila kupingwa,hivyo wao watumishi wa RBF wamejipanga kwa kuandaa Mpango Kazi sambamba na kuainisha manunuzi yote kwenye mfumo wa NeST,ili kuanza utekelezaji wa bajeti hiyo ifikapo Julai 1,2025.