Mwamvua Mwinyi, Bagamoyo
Februari 2, 2025
Wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wapatao 52 kutoka Wilaya ya Bagamoyo, Mkoani Pwani, wamejitokeza kuchukua fomu za kuwania nafasi ya Mwenyekiti wa chama hicho wilayani humo.
Hatua hii imechukuliwa kufuatia kuzibwa kwa nafasi hiyo baada ya Mwenyekiti wa awali, Alhaj Abdul Sharif Zahoro, kuondolewa kutokana na kukiuka maadili ya uongozi na Kamati Kuu ya CCM Taifa iliyofanya maamuzi hayo katika kikao maalum kilichofanyika tarehe 1 Septemba 2024.
Akizungumzia kumalizika kwa zoezi hilo, Katibu Mwenezi wa Wilaya ya Bagamoyo, Ramadhani Lukanga, alieleza kuwa zoezi hilo linahusisha kuchagua Mwenyekiti atakayechukua nafasi ya Abdul Sharif, ambaye ametenguliwa na uongozi wa CCM Taifa.
Alieleza, kati ya wanachama hao waliochukua fomu, 46 walirejesha fomu zao kabla ya kufika mwisho wa zoezi hilo tarehe 28 Januari mwaka huu.
“Kamati ya Siasa inawapongeza wanachama wote waliochukua fomu, wametimiza demokrasia, Hatua inayofuata ni kupanga tarehe ya kukutana ili kupitia majina ya wagombea kabla ya kuyapeleka Mkoani na Ngazi ya Taifa kwa ajili ya mchujo,” alisisitiza Lukanga.
Lukanga alitoa wito kwa wanachama wa CCM wilayani Bagamoyo kuwa na utulivu na kuvuta subira wakati vikao vikipitia majina ya wagombea, baada ya hapo, uchaguzi wa kumpata mrithi wa nafasi hiyo utaandaliwa.
“Zoezi la uchukuaji wa fomu na mchakato mzima wa kuchuja na kupiga kura linahusisha wanachama wanaogombea pamoja na wapambe wao, Hivyo, tunawaasa wanachama baada ya vikao na kumtangaza Mwenyekiti mpya tuvunje makundi na kuendeleza umoja wetu,” alisisitiza Lukanga.
Mwenyekiti aliyetenguliwa, Alhaj Abdul Sharif, aliiongoza CCM Wilaya ya Bagamoyo kwa vipindi viwili kabla ya Kamati Kuu ya CCM Taifa kuamua kumuondoa kwenye nafasi hiyo.
Viongozi wengine waliotenguliwa septemba 1 2024 ,ni pamoja na Paline Ninje, aliyekuwa Mwenyekiti wa UWT Lindi, na Munira Nkango, aliyekuwa Mwenyekiti wa UVCCM Singida.
