Tume ya Ushindani (FCC) imejizatiti kuelimisha Watanzania kuhusu mbinu bora za kufanya biashara bila kukiuka sera na taratibu za ushindani, ndani na nje ya mipaka ya nchi.
Mkurugenzi Mkuu wa FCC, William Erio, alieleza hayo Ijumaa, Novemba 29, 2024, katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika ofisi za FCC, Dar es Salaam. Tukio hilo lilihusisha uzinduzi wa Maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Ushindani Duniani, yanayotarajiwa kufikia kilele Desemba 5, 2024.
Erio alibainisha kuwa mazingira ya biashara yanahitaji kudhibitiwa kupitia sera na sheria ili kuhakikisha ushindani wa haki. Alitoa mfano wa mikataba inayokinzana na ushindani na miungano ya kampuni inayodhoofisha ushindani kama changamoto zinazohitaji kudhibitiwa.
“Licha ya mfumo wa biashara huria, kuna tofauti za rasilimali kati ya wafanyabiashara. Bila udhibiti, kampuni kubwa zinaweza kutumia nguvu zao za kifedha, rasilimali watu, au utaalamu kuwatoa washindani sokoni, hali inayozuia fursa sawa kwa wote,” alisema Erio.
Aliongeza kuwa baadhi ya wafanyabiashara hutumia mbinu zisizo za haki ili kutawala soko, jambo linaloweza kuathiri upatikanaji wa bidhaa na huduma huku wakilenga kuongeza faida kwa gharama ya ushindani.
FCC, kama taasisi, imeweka mikakati ya kuhakikisha mazingira sawa ya biashara kupitia utekelezaji wa sera na sheria za ushindani.
Maadhimisho hayo yatahitimishwa Desemba 5, 2024, katika Hoteli ya Golden Tulip, Oysterbay, Dar es Salaam. Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Selemani Jafo, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi. Kilele hicho kitajumuisha kongamano litakalowakutanisha wataalam wa sheria na biashara, ambapo watajadili mazingira ya biashara na ushindani nchini, huku wakitoa ushauri kwa FCC kuhusu utekelezaji bora wa majukumu yake.
Maadhimisho haya yanafanyika chini ya kaulimbiu “Sera ya Ushindani na Kudhibiti Kukosekana kwa Usawa katika Uchumi.”