Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha,Missaile Musa akizungumza  wakati akifungua mafunzo kwa wataalamu wa manunuzi na Ugavi  mkoani Arusha.
Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya wataalamu wa ununuzi na ugavi hapa nchini(PSPTB)Godfred Mbanyi  akizungumza kwenye semina hiyo inayoendelea mkoani Arusha.
………..
Happy Lazaro,Arusha .
WATAALAMU wa ununuzi na Ugavi   nchini wametakiwa kuwa  waadilifu na weledi  katika utendaji kazi wao huku wakitanguliza  uzalendo pamoja na kuzingatia kanuni na taratibu katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku .
Hayo yamesemwa leo mkoani Arusha na Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha,Missaile Musa  wakati akifungua mafunzo kwa wataalamu wa manunuzi na Ugavi  ambayo yameandaliwa na Bodi ya wataalamu wa ununuzi na ugavi(PSPTB)na kushirikisha wataalamu wa sekta hiyo toka halmashauri zote na sekretarieti ya mkoa wa Arusha.
Aidha amewataka kuzingatia misingi ya taaluma yao kwani taaluma hiyo ya ununuzi na Ugavi ni kubwa sana na lazima waitendee  haki kwa kufuata maadili ya kazi hiyo na kuweza kuwa mfano wa kuigwa. 
“Kupitia mafunzo haya kutasaidia sana kukumbushwa  wajibu  wenu kuhusu michakato  ya manunuzi ili ipatikane  bila ucheleweshaji kwani nimeambiwa kuwa mtaweza kujifunza sheria  mpya ya ununuzi na Ugavi ambayo inaelekeza weledi na usimamizi wa fedha za serikali. “amesema .
Aidha Musa  amewataka kujiepusha na vitendo vya rushwa na kujikita zaidi katika kusimamia kikamilifu fedha zote za umma   zinazotengwa kwa ajili ya  miradi mbalimbali.
“hakikisheni mnajifunza   kwa umakini mkubwa kuandaa na kutunza mikataba,na mzingatie yaleyote mnayofunzishwa hapa ili mkitoka muende mkayatekeleze kwa vitedo”alisisitiza katibu Tawala huyo wa Mkoa.
Awali Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya wataalamu wa ununuzi na ugavi hapa nchini(PSPTB)Godfred Mbanyi amesema kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo wataalamu hao juu ya sheria mpya ya ununuzi na namna ya kusimamia mikataba.
Amesema kuwa changamoto kubwa wanayokumbana nayo katika maeneo mengi hapa nchini ni wataalamu wa ununuzi kufanya kazi pasipo kusajiliwa na bodi hyo jambo ambalo ni kinyume cha sheria na kuwataka wale wote ambao hawajasajiliwa wajisajili mara moja.
“Natoa wito kuzingatia sheria kanuni na taratibu za manunuzi katika kutekeleza majukumu yenu,na nawataka wale wote ambao hawajasajiliwa na bodi kujisajili haraka iwezekanavyo kwani iko kwa mujibu wa sheria na anayefanya kazi bila kusajiliwa anavunja sheria za nchi”amesema Mbanyi.
Kwa upande wake Mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo,Catherine Mwamasage ambaye ni Mkuu wa kitengo cha manunuzi kutoka TANAPA,amepongeza PSPTB kwa kuwapatia mafunzo hayo na kusema kuwa yatawasaidia kupata maarifa zaidi na wataenda kuyafanyia kazi kwa vitendo.
Aidha mafunzo hayo ya siku mbili yameandaliwa na Bodi ya wataalamu wa ununuzi na ugavi(PSPTB)na kushirikisha wataalamu wa sekta hiyo toka halmashauri zote na sekretarieti ya mkoa wa Arusha.