Timu ya kata ya Mecco imeyaaga mashindano ya mpira wa miguu ya The Angeline Jimbo Cup 2024 baada ya kukubali kipigo cha magoli mawili kwa moja kutoka kwa timu ya kata ya Ibungilo
Akizungumza mara baada ya kuisha kwa mchezo wao uliofanyika katika viwanja vya shule ya msingi Sabasaba nahodha wa timu ya kata ya Mecco Evocado Lucas amesema kuwa timu yake ilianza kucheza vizuri kwa kufuata maelekezo ya mwalimu na kushinda goli la kwanza katika kipindi cha kwanza licha ya kuwa na wachezaji pungufu kwa muda lakini baada ya kipindi cha pili walifanya makosa na ndio yaliyowagharimu kiasi cha kufungwa magoli mawili mfululizo
‘.. Tulianza kucheza kwa morali na kwa mafanikio makubwa lakini mara baada ya kipindi cha pili kuanza tulibweteka tukaacha kucheza kwa morali na maarifa makubwa hivyo wenzetu kutumia nafasi hiyo kurudisha goli tulilowafunga na baadae kutuongeza goli jengine ..’ Alisema
Aidha nahodha huyo amemshukuru Mbunge wa Ilemela Dkt Angeline Mabula kwa kuasisi mashindano hayo pamoja na kuwaahidi mashabiki wa timu yake kujiandaa vizuri na kufanya vyema katika msimu ujao wa mashindano hayo
Juma Selemani ni nahodha wa timu ya kata ya Ibungilo ambapo amesema kuwa walianza kucheza kwa kuridhika bila mafanikio kwa kipindi cha kwanza lakini baada ya kuanza kwa kipindi cha pili walibadilika na kuanza kucheza kama timu iliyowahi kuchukua ubingwa wa mashindano hayo miaka kadhaa huko nyuma hivyo kurudisha goli walilokuwa wamefungwa na baadae kuongeza jengine lililowafanya kufuzu hatua ya robo fainali
Mashindano ya The Angeline Jimbo Cup msimu wa nane kwa mwaka 2024 yataendelea hapo kesho kwa kuzikutanisha timu ya kata ya Nyamhongolo dhidi ya timu ya waendesha bajaji kufuzu hatua ya robo fainali huku yakipambwa na kauli mbiu ya ‘Uchaguzi wa serikali za mitaa 2024, Ilemela tunaanzia tulipoishia’