Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe Albert Chalamila Leo Septemba 3,2024 amekutana na Kamishna Mkuu wa TRA Bw.Yusuph Mwenda akiongozana na baadhi ya wataalamu wa mamlaka hiyo katika kikao kilichofanyika ofisi ya Mkuu wa Mkoa Ilala Boma.
RC Chalamila ametoa shukrani kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kutambua umuhimu wa taasisi hii katika kusaidia maendeleo ya mapato Nchini na kupanua wigo wa walipa kodi hususani katika Mkoa wa Dar es salaam.
Katika kikao hicho Mhe.Chalamila ameongelea mambo kadhaa yaliyojadiliwa ikiwa ni kupunguza migogoro ya kikodi inayolalamikiwa na wafanyabiashara,kutanua wigo kwa walipa kodi kulingana na vyanzo vingi vya mapato vilivyopo katika Mkoa huu na pia kuboresha miundombinu ya kikodi ili TRA iweze kukusanya mapato zaidi.
Aidha RC Chalamila amezungumzia umuhimu wa TRA kurejesha pato lake kiasi kwa ajili ya kuweza kuboresha miundombinu ya kijamii (CSR)kama vile shule na vitu vinginevyo katika Mkoa huu.
Kwa upande wake Kamishna Mkuu wa TRA amemshukuru Mhe Chalamila kwa ushirikiano anaoutoa kwa kufanya kazi na mamlaka ya mapato Tanzania kwa wilaya zote tano za Dar es salaam na kuthibitisha kuwa Dar es salaam ni kitovu cha biashara kwa kuwa inakusanya kodi zake zote kwa asilimia takribani 80%.
Mwisho RC Chalamila amepongeza timu ya Mamlaka ya Mapato Tanzania kwa kuahidi ushirikiano ili kuboresha namna ya kuuendeleza katika wilaya zote na maeneo yote ya biashara kuimarika kwa kutatua changamoto zilizopo pia kuendelea kutoa elimu ya kodi kwa umma.