NA FAUZIA MUSSA

WAKALA wa Chakula na Dawa ,  Zanzibar (ZFDA) imeyafungia maduka manne ya bidhaa za nyama (mabucha) kutokana na kwenda kinyume na  taratibu za kuendeshea biashara hiyo.

Mkuu wa Kitengo cha Ukaguzi wa bidhaa za mifugo Dk.Thamra Khamis Talib alieleza hayo mara baada ya kufanya ukaguzi  katika maduka  yaliopo maeneo ya Mkoa wa Mjini Magharibi.

Alisema Taasisi hiyo inaendesha zoezi hilo mara kwa mara na kuchuka hatua mbalimbali kwa maduka ambayo yatabainika kwenda kinyume na taratibu zilizowekwa na wakala huo ili kuhakisha bidhaa hizo zinabaki kuwa  salama kwa matumizi ya  binaadamu.

“Tunafanya ukaguzi huu ili kuhakikisha maduka  yote  ya nyama  yanasajiliwa, yapo katika  hali ya usafi, vifaa wanavyotumia  ni sahihi ikiwemo misumeno ya moto na kuangalia  afya za  wahudumu  wa maduka  hayo kwa Lengo la  kumlinda mtumiaji  wa bidhaa hiyo, ” alifahamisha Dk.Thamra

 Aidha aliwataka wafanyabiashara  kufuta miongozo inayotolewa na wakala huo ikiwemo kupima afya, kusajili maduka na kudumisha usafi ili kumlinda mtumiaji wa mwisho wa bidhaa hiyo.

Alifahamisha kuwa licha ya juhudi wanazozichukua lakini bado wapo baadhi ya wafanyabiashara wa bidhaa hiyo wanaokwenda kinyume na utaratibu wa ZFDA jambo linalohatarisha afya za wananchi.

“Kati ya mabucha 15  – 20 tunayoyapitia ni mabucha matatu mpaka manne  ndio yanayokidhi  vigezo na masharti ya ZFDA” alieleza

Alisema hali hiyo inatokana na uelewa mdogo wa wafanyabiashara hao kwani wengi wao wanaangalia kipato na sio afya za watumiaji.

Aidha alieleza kuwa ZFDA itaendelea kuwachukulia hatua wafanyabiashara wote wanaokwenda kinyume na taratibu za taasisi hiyo ikiwa ni pamoja na kuyafungia maduka yao  hadi pale watakapofuata taratibu hizo.

Mbali na hayo aliwataka wafanya biashara hao kufika ZFDA kupata elimu na miongozo ya   ya kuendesha biashara hiyo  ili  kuepuka kuingia makosani.

Baadhi ya wafanyabiashara wa bidhaa hiyo akiwemo Juma Ali Vuai wa Kibandamaiti na Sleiman Hamad wa  Jang’ombe waliahidi kufuata taratibu katika  makosa waliobainika  kuwa nayo ili kuwa salama katika kazi zao.

Miongoni mwa watumiaji wa bidhaa hiyo Mafunda Said Ali aliwashauri wafanyabiashara hao kuwa wazalendo  na kujali afya za watumiaji badala ya  maslahi binafsi na kuwasisitiza kudumisha usafi kwani ndio kivutio kikubwa cha wateja .

Hata hivyo walisema jukumu la kulinda afya linaanza kwa mtumiaji mwenyewe hivyo waliwashauri watumiaji kuangalia usafi wa muuzaji ,mazingira ya bidhaa yenyewe kabla ya kununua ili kulinda afya zao.

“Tunze kuzijali afya zetu sisi wenyewe tuhakikishe tunanunua bidhaa katika maduka  ambayo ni masafi, wauzaji wake ni wasafi ili kulinda afya zetu, na hii inaweza kusaidia baadhi ya wafanyabiashara kubadilika na kudumisha usafi” alieleza 

Katika ukaguzi huo ZFDA wamekagua maduka ya nyama  maeneo ya Mombasa,Jang’ombe ,Amani,  Magomeni na Kibandamaiti.