Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera,Bunge na Uratibu Mheshimiwa Jenista Mhagama akizungumza kabla ya kuzindua  mradi wa ARSNA katika kijiji cha Mpitimbi wilayani Songea mkoani Ruvuma unaotekelezwa katika mikoa ya Ruvuma na Lindi kwa gharama ya shilingi bilioni 3.1.
Baadhi ya wananchi wakiwa kwenye mradi wa shamba darasa la  mabwawa ya ufugaji samaki katika kijiji cha Mpitimbi kwenye hafla ya uznduzi wa mradi iliyofanywa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Mheshimiwa Jenista Mhagama ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Peramiho wilayani Songea mkoani Ruvuma.
Baadhi ya wananchi katika kijiji cha Mpitimbi wilayani Songea mkoani Ruvuma wakishuhudia uzinduzi wa mradi wa ARSNA uliofanywa na Waziri Jenista Mhagama kwenye shamba darasa la mabwawa ya ufugaji samaki katika kijiji cha Mpitimbi wilayani Songea.
……….

Na Albano Midelo,Songea

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera,Bunge na Uratibu  Mheshimiwa Jenista Mhagama amezindua mradi wa kuendeleza lishe na ufugaji endelevu wa viumbe maji kwa wakulima wadogo (ARSNA)  unaogharimu  shilingi bilioni 3.1 katika Kijiji cha Mpitimbi wilayani Songea mkoani Ruvuma.

Waziri Mhagama amesema mradi huo unaotekelezwa na serikali katika mikoa ya Ruvuma na Lindi kwa unafadhiliwa na serikali ya Norway kupitia Shirika la NORAD na kwamba unatekelezwa   kwa kipindi cha miaka miwili kuanzia Machi 2024 hadi Machi 2026.

 Ameutaja mradi huo kuwa umelenga kuleta mabadiliko makubwa kwenye uzalishaji na uendelezaji wa biashara ya ufugaji Samaki na uzalishaji wa mwani kwa lengo la kuwawezesha  wananchi kunufaika katika maeneo yao ufugaji Samaki na uzalishaji wa mwani.

Amesema serikali imekusudia kuendeleza kilimo na uvuvi katika mikoa ya Ruvuma,Lindi ili kupata mafanikio makubwa na kuongeza tija na kukabiliana na  changamoto kubwa  ya upatikanaji wa vifaranga vyenye ubora na chakula cha Samaki.

“Kupitia mradi huu wazalishaji binafsi wa  vifaranga vya samaki watajengewa uwezo katika uzalishaji wa vifaranga na wafugaji wa Samaki hususan vijana watajengewa uwezo  wa kutengeneza chakula cha Samaki ’’,alisisitiza Mhagama.

Waziri Mhagama amesema tayari serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imejenga shamba darasa la ufugaji wa samaki katika Kijiji cha Mpitimbi ambalo amesema litakuwa chachu kubwa katika ufugaji bora wa Samaki ambapo amewaomba wananchi hao kutumia shamba darasa hilo ili kuongeza tija katika ufugaji wa Samaki.

Ametoa rai kwa wakuu wa mikoa ya Ruvuma na Lindi ambako mradi  huo unakwenda kutekelezwa  kuhakikisha mradi unakwenda kutekelezwa kwa ufanisi mkubwa  ili kupata tija na thamani halisi ya fedha zitakazotumika.

Awali akitoa taarifa ya mradi huo Naibu Katibu Mkuu  Ofisi ya Waziri Mkuu Sera,Bunge na Uratibu Underson Mutatembwa ameutaja mradi wa  ARSNA  kuwa unataarajia kuzifikia kaya 5,000 za wakulima wadogo  ikijumuisha wanawake asilimia 50 vijana asilimia 40 na makundi mengine asilimia 10.

Amesema mradi huo unaogharimu shilingi bilioni 3.1 unatekelezwa katika kipindi cha miaka miwili kuanzia Machi 2024 hadi Machi 2026 katika Halmashauri za Wilaya ya Songea na Mbinga mkoani Ruvuma na Halmashauri za Wilaya  za Mtama na Ruangwa mkoani Lindi .

Amesema Tanzania imekuwa moja ya nchi  tatu za Afrika  zilizopata fursa ya kunufaika na utekelezaji wa mradi huu nchi nyingine amezitaja kuwa ni Msumbiji na Kenya  na kwamba mradi huo ni sehemu ya utekelezaji wa program kubwa ya kuendeleza kilimo na uvuvi inayofadhiliwa na Shirika la IFAD inayotekelezwa katika mikoa 12 ya Tanzania kwa gharama ya  shilingi bilioni 150.

Akizungumza kwenye uzinduzi huo Mwakilishi wa Mkurugenzi  IFAD  Afrika Mashariki na Kusini  Jacquiline Machangu  amesema IFAD imekuwa ikifanya kazi na Serikali ya  Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwemo sekta ya kilimo hususan wakulima wadogo waliopo vijijini.

Amesema IFAD  kupitia mradi wa ARSNA  imelenga kuongeza mapato na kujenga uwezo kimaisha wafugaji wadogo katika maeneo matatu.

Ameyataja maeneo hayo kuwa ni ongezeko la uzalishaji na ustahimilivu kwa wafugaji wadogo wa Samaki,kuongeza kwa fursa  kwa wanawake na vijana kupitia ubunifu kwenye masoko  na kuendeleza ujuzi na uundaji wa sera mpya.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mheshimiwa Alexander Mnyeti  akizungumza kwenye uzinduzi huo amesema  Wizara hiyo itaendelea kutoa watalaam wa uvuvi ili kufanikisha mradi huo unakwenda kuzalisha Samaki wengi kwenye mabwawa ambao  wana virutubisho muhimu.

Amesema Samaki wa mabwawa wanaweza kumaliza changamoto ya udumavu kwenye Mkoa wa Ruvuma ambapo hivi sasa udumavu umefikia asilimia 37 katika Mkoa wa Ruvuma , licha ya Mkoa huo kutajwa kuwa ni ghala la chakula nchini.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Ahmed Abbas Ahmed  ameishukuru serikali kwa kuanza kutekeleza mradi huo mkubwa wa ufugaji Samaki katika Kijiji cha Mpitimbi.

Hata hivyo amesema serikali imekuwa inatekeleza miradi mikubwa katika jimbo la Peramiho ukiwemo mradi wa ujenzi wa barabara ya lami nzito kutoka Likuyufusi hadi Mkenda mpakani mwa Tanzania na Msumbiji.

Amesema mradi huo upo mbioni kuanza kutekelezwa serikali imetenga shilingi bilioni 74 kuanza kujenga lami kilometa 60 na kwamba serikali imetoa mabilioni ya fedha kutekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati mkoani Ruvuma.

Ameitaja baadhi ya miradi iliyotekelezwa kuwa  ni ujenzi wa barabara ya lami nzito kilometa 66 kutoka Mbinga hadi Mbambabay kwa gharama ya shilingi bilioni 127,ujenzi wa bandari ya kimkakati ya Ndumbi kwa gharama ya  Zaidi ya shilingi bilioni 12 na ukarabati wa uwanja wa ndege Songea kwa gharama ya shilingi bilioni 37.