Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi akifungua jengo la Dawati la Jinsia wilayani humo leo kwa kukata utepe.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza,Wilbrod Mutafungwa akitoa takwimu za ukatili leo wakati kabla ya kufunguliwa jengo la Dawati la Jinsia la Wilaya ya Nyamagana.
Mwonekano wa jengo la ofisi za Dawati la Jinsia Polisi Wilaya ya Nyamagana ambalo limejengwa na Shirika la SOS children’s Villages lishikirikiana na The Desk & Chair Foundation pamoja na KIVULINI kwa gharama ya sh. milioni 66.5.
…………….

NA BALTAZAR MASHAKA,MWANZA

KAMANDA wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbrod Mutafungwa ameanika takwimu za matukio ya ukatili wa kijinisia mkoani humu zikionesha ubakaji,mimba kwa wanafunzi wa kike na ulawiti yanaongoza.

Ametoa takwimu hizo leo wakati wa  ufunguzi wa jengo la Dawati la Jinsia la Wiliya ya Nyamagana,lililojengwa na Shirika la SOS Children’s Villages kwa gharama ya sh. milioni 66.5 likishirikiana na The Desk & Chair Foundation pamoja na KIVULINI.

Mutafungwa amesema tangu kuanzishwa madawati ya Jinsia mwitikio wa wananchi kutoa taarifa za ukatili na uhalifu,umeongezeka na matukio sasa hayafichwi,hatua zinachukuliwa dhidi ya watuhumiwa.

“Madawati ya jinsia yanawapa faragha waathirika wa ukatili,yanawawezesha kutoa taarifa za ukatili waliofanyiwa kwa kutulia, wanahudumiwa kwa usiri na askari wenye weledi waliopitia mafunzo ya namna ya kuwahudumia,hivyo jengo hili lina umuhimu wa pekee,”amesema.

Mutafungwa amesema ingawa serikali inapambana kudhibiti vitendo vya ukatili bado matukio ya ubakaji na ulawiti yapo,takwimu zinaonesha tangu mwaka juzi hadi Aprili mwaka huu,makosa ya ubakaji yanaongoza kwa matukio 537, mimba kwa wanafunzi wa kike 534 na ulawiti matukio 197.

“Mwaka 2022  matukio ya  ubakaji yalikuwa 235,mwaka 2023 (254),na matukio 48 ya 2024 hadi Aprili pia,kundi la wanafunzi wa kike liliendelea kuandamwa na ukatili wa kingono,mwaka 2022  mimba kwa wanafunzi zilikuwa 284,mwaka 2023 (95),mwaka huu  hadi Aprili (54),”ameeleza Mutafungwa.

Ameeleza kuwa ulawiti kwa kipindi cha mwaka juzi hadi Aprili 2024 yaliripotiwa matukio 197 ambapo mwaka 2022 (91),mwaka 2023 (84) na mwaka 2024 (22),pia matukio jumla ya 160 ya  ukatili kwa watoto yaliripotiwa,mwaka 2022 (72),mwaka 2023 (63),na mwaka 2024 (25).

Kwa mujibu wa Mutafungwa matukio ya kutelekeza jumla yalipokelewa 131,kwa mwaka 2022 (68),mwaka 2023 (48) na  mwaka huu (15) pia, wanafunzi jumla ya 69 walitoroshwa,mwaka 2022 (31), mwaka 2023 (30) na mwaka huu hadi Aprili (8).

Pia,kutupa watoto kulikuwa na jumla ya matukio 43,mwaka 2022 (16), mwaka 2023 (19) na matukio 8 ya hadi Aprili mwaka huu,watoto kuibwa jumla ya taarifa 35 zilipokelewa, mwaka 2022 (16) sawa na mwaka 2023 ambapo matatu yalikuwa ya hadi Aprili mwaka huu, huku matukio ya kuzini na ndugu (maharimu) yakiripotiwa 16 kati ya hayo mwaka 2022 (8), mwaka 2023 (6) na mwaka huu (2) hadi Aprili.

Naye Mratibu wa Mpango wa kuimarisha familia, Elizabeth Swai kwa niaba ya Mkurugenzi wa SOS Children’s Villages,linalohudumia watoto walio katika hatari ya kupoteza malezi na waliopoteza malezi, Florian Fanuel,amesema wamechangia asilimia sh.milioni 58 sawa na asilimia 83.7 ya sh.milioni 66.5 katika ujenzi huo zikiwemo sh. milioni 2.4 za vitanda vinne na magodoro baada ya ujenzi kukamilika.

“SOS Children’s Villages inashirikiana na serikali kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia katika jamii, hivyo wanaamini kupitia uwekezaji huo watoto watapata haki zao mashauri yao yatashughulikiwa kwa usiri kisha kupelekwa mahakamani,aliiomba jamii kuendelea kufichua vitendo vya ukatili wanavyofanyiwa watoto kuanzia  ngazi ya familia,”amesema Swai na kuongeza;

“Dawati la Jinsia Wilaya ya Nyamagana linaloshughulikia masuala ya ukatili dhidi ya watoto na wanawake halikuwa na usiri,lilikuwa na chumba kimoja chenye mwingiliano wa watu,hivyo wathirika hawakuwa  na faragha wala uhuru wa kutoa taarifa za ukatili waliofanyiwa,tukaona vyema kujenga ofisi hii.”

Amesema wanawake na watoto wanaofanyiwa ukatili kupitia jengo hilo watahudumiwa kwa usiri na kubaki salama,jamii pia itabaki salama baada ya watuhumiwa kuchukuliwa hatua.

Aidha,SOS Children’s Villages wanatoa elimu kwa jamii kupitia kamati za MTAKUWWA ili kuimarisha ulinzi wa watoto na kuhakikisha usalama wao unakuwepo kwenye ngazi hizo,kaya hadi katika jamii kuhakisha taarifa za ukatili zinazoibuliwa na jamii zinazotolewa na kushughulikiwa.

Akifungua jengo hilo la kisasa,Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana,Amina Makilagi amesema Shirika la SOS Chidren’s Villages Tanzania,limejitoa kwa dhati katika kuunga mkono jitihada za serikali kudhibiti ukatili wa kijinsia kwa vitendo.

Amepongeza uwekezaji wa jengo la ofisi za Dawati la Jinsia la Wilaya ya Nyamagana,lililogharimu sh.milioni 66.5 huku shirika likichangia fedha sh.milioni 55.6 kati ya sh.milioni 66.5,kujenga ofisi za dawati hilo wilayani humo fedha ambazo zingeleta maendeleo katika huduma nyingine za jamii.

Makilagi amesema elimu inayotembea ya kupinga ukatili huo imewezesha taarifa za vitendo hivyo kuongezeka baada ya madawati ya jinsia kuimarishwa,wananchi wamefahamu athari za vitendo hivyo na kuitaka jamii kubadilika na kuwa watu wema wanaocha Mungu na kuzingatia maadili.

“Vitendo vya ubakaji,ulawiti na mimba kwa wanafunzi vinaendelea kufanyika,rai yangu jamii ivikemee kuwa haviwezekani kwa sababu vinakiuka maadili,vinatweza na vinadhalilisha utu na hivyo watii sheria na kumcha Mungu ili kuvitokomeza,” amesema mkuu huyo wa wilaya.

Ameonya wenye tabia ya kutenda na kuendeleza vitendo vya ukatili dhidi ya watoto na wanawake kuwa,serikali imejipanga kimkakati,vikizidi kutokea katika familia na jamii,watu wasivifumbie macho, wasiwafiche wahusika na wawe tayari kutoa ushahidi mahakamani wawajibe kisheria.