MSEMAJI  wa familia ya Hayati Sokoine Bw. Lembris Kipuyo,akizungumza  na waandishi wa habari leo Machi 28,2024 jijini Dodoma kuhusu kumbukizi ya miaka 40 ya Hayati Edward Moringe Sokoine, aliyekuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, itakayofanyika Aprili 12, 2024, katika Kijiji cha Enguik, Monduli Juu mkoani Arusha.

Na.Alex Sonna-DODOMA

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan, atarajiwa kuwaongoza viongozi mbalimbali pamoja na baadhi ya Watanzania kwenye ibada maalum ya kumbukizi ya miaka 40 ya Hayati Edward Moringe Sokoine, aliyekuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, itakayofanyika Aprili 12, 2024, katika Kijiji cha Enguik, Monduli Juu mkoani Arusha.

Hayo yamesemwa leo Machi 28,2024 jijini Dodoma na  Msemaji wa familia ya Hayati Sokoine Lembris Kipuyo,wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Amesema kuwa  ibada hiyo itafanyika Aprili 12, 2024, saa 3:00 asubuhi, ambapo imeandaliwa na familia ikishirikiana na Taasisi ya Hayati Edward Moringe Sokoine.

“Ibada hiyo ya kumbukumbu ya Hayati Sokoine itawashirikisha viongozi mbalimbali wa serikali wakiongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.”amesema Bw.Kipuyo

Aidha ameeleza  lengo la kuanzishwa kwa Taasisi ya Hayati Edward Moringe Sokoine, ni kuenzi mema aliyoyafanya kwani aliacha alama kubwa ambayo taifa linamkumbuka hadi leo.

Hata hivyo amesema kuwa Taasisi hiyo imejikita katika masuala ya elimu, kilimo, hifadhi ya mazingira, vyanzo vya maji pamoja na afya.

Kipuyo, amesema kuwa  Hayati Sokoine alifanya mambo makubwa sana katika Taifa la Tanzania ambayo hadi leo yameacha alama kubwa hivyo kupitia siku hiyo Watanzania watapata fursa ya kuelewa kile alichokifanya wakati wa uhai wake.

‘Hayati Sokoine alikuwa mzalendo wa kweli, alipenda taifa lake na wananchi wake, alihakikisha kwamba rasilimali za nchi zinatumika na Watanzania wote, aliwatumikia wananchi bila kubagua na alikuwa na hofu ya Mungu katika kufanya kazi zake”amesema 

Hayati Sokoine alikuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika vipindi viwili wakati wa uongozi wa Awamu ya Kwanza. Alizaliwa Agosti 01, 1934, kijijini Enguik, Monduli Juu wilayani Monduli, mkoani Arusha.