Wahitimu wa mafunzo ya ufundi katika chuo cha ufundi stadi Kiuma wilayani Tunduru wakiwa katika maandamano kabla ya kufanyika kwa mahafali ya 25 ya chuo hicho.
Mwanafunzi wa fani ya umeme wa majumbani kutoka chuo cha ufundi stadi Kiuma ambaye hakufahamika jina lake mara moja,akionyesha namna ya kuunganisha umeme majumbani kwenye mahafali ya 25 ya chuo hicho,kulia ni mgeni rasmi katika mahafali hayo meneja wa Temesa mkoa wa Ruvuma Mhandisi Frank Jackson na kulia kwake Mkuu wa chuo Robert Makwenda.
Mkuu wa chuo cha ufundi Stadi -Kiuma kilichopo kijiji cha Milonde kaya ya Matemanga wilayani Tunduru Robert Makwenda akitoa taarifa ya chuo hicho kwenye mahafali ya 25 iliyofanyika katika viwanja vya Kiuma.
Katibu Mkuu wa Taasisi ya Kiuma Daniel Malukuta,akitoa salamu za taasisi hiyo kwa wahitimu wa mafunzo ya ufundi na wazazi kwenye mahafali ya 25 ya chuo cha ufundi stadi Kiuma.
….
Na Muhidin Amri, Tunduru
JUMLA ya vijana 85 wakiwemo wavulana 71 na wasichana 14 wamehitimu elimu ya mafunzo ya ufundi stadi katika Chuo cha Ufundi Kiuma kilichopo kijiji cha Milonde kata ya Matemanga wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma.
Akizungumza na wahitimu hao kwenye mahafali ya 25 ya chuo hicho, Meneja wa wakala wa ufundi na umeme(TEMESA)Mkoa wa Ruvuma Mhandisi Frank Jackson amewataka kutumia vizuri ujuzi walioupata kuleta ufumbuzi wa changamoto zilizopo katika jamii na kutafuta ajira kwenye sekta isiyo rasmi ili kujiletea maendeleo.
Alisema,hakuna shaka kuwa chuo cha ufundi Kiuma ni miongoni mwa vyuo bora hapa nchini vinavyotoa elimu ambayo kama ikizingatiwa kikamilifu kinatoa fursa ya kujiajiri na kuajiriwa na chachu ya maendeleo katika nyanja mbalimbali.
“serikali kupitia ofisi ya wakala wa ufundi na umeme (Temesa)itaendelea kushirikiana na chuo hiki kwa kuwapokea wanafunzi watakaoletwa kwa ajili ya mafunzo kwa vitendo kwa ajili ya kuwaanda ili waweze kutimiza ndoto zao za kujiajiri na kuajiriwa baada ya kumaliza mafunzo yao”alisema Mhandisi Jackson.
Amewaasa wahitimu hao kuwa wazalendo,waaminifu,waadilifu kwa nchi yao,kufanya kazi kwa bidii na kwa weledi mkubwa na kuzitumia vizuri fursa zilizopo hususani katika sekta ya binafsi kwa kujipatia kipato na kutoa mchango wao kwa Taifa badala ya kuwa sehemu ya kundi la walalamikaji.
Kwa upande wake katibu Mkuu wa Taasisi ya Kiuma Daniel Malukuta alisema,wataendelea kushirikiana na serikali ili kufikia lengo la kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda kwa kuzalisha vijana wengi wenye ujuzi katika fani mbalimbali.
Malukuta,ameishukuru serikali kwa namna inavyoshirikiana na Taasisi ya Kiuma katika nyanja za kiroho na kijamii na kueleza kuwa,hilo ni jambo linalopaswa kuendelezwa kwa manufaa ya Watanzania wote bila kujali itikadi za Dini.
Aidha amewataka wahitimu,kuwa mfano mzuri kwa jamii mara baada ya kumaliza mafunzo katika chuo hicho na kuwa waaminifu na wakweli watakapokuwa wanatekeleza majukumu yao na kuwa mabalozi wazuri wa chuo cha ufundi na taasisi ya Kiuma kwa ujumla.
Naye Mkuu wa chuo hicho Robert Makwenda,amewaomba wazazi na walezi kuwapeleka vijana wao kupata ujuzi katika fani za ujenzi,useremala,uchomeaji uungaji vyuma,ufundi wa magari,umeme,ushonaji nguo na kozi fupi ya kompyuta.
Alisema,hatua hiyo itasaidia kupunguza kundi la wazururaji,kukaa vijiweni na baadhi yao kujihusisha na makundi hatarishi kama watumiaji wa dawa za kulevya ambayo yanachangia sana kupungua kwa nguvu kazi ya Taifa.
Pia alieleza kuwa,wanatoa mafunzo ya ufundi katika vituo vya matumaini ambavyo ni Kidodoma, Amani, Twendembele, Kalulu na Namtumbo kwa lengo la kuwapunguzia gharama kutokana na jukumu lao kama chuo cha ufundi Stadi.
Alisema,pamoja na gharama za kuendeshea mafunzo kuwa kubwa,uongozi wa kituo ukishirikiano na uongozi wa chuo,wanachuo wanaosoma Kiuma VTC wanapata ofa ya huduma ya chakula na bweni bila malipo kwa muda wote wa mafunzo yao.
Wahitimu wa chuo hicho kupitia risala yao iliyosomwa na Omari Elimu,wameipongeza taasisi ya Kiuma kuongeza wakufunzi waliowapa ujuzi ambao watakwenda kuutumia katika shughuli zao za kujiletea maendeleo.
Hata hivyo,wameiomba taasisi hiyo kupitia uongozi wa chuo kuongeza vifaa vya kujifunzia na kufundishia ili kupanua wigo wa kitaaluma na kuomba kupatiwa ajira kwenye idara zilizochini ya taasisi ya Kiuma.