Naibu Waziri wa Uchukuzi David Kihenzile akizungumza kwenye hafla ya utiaji saini wa mikataba ya ukarabati wa meli tatu na uzinduzi wa meli ya Mv Umoja.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya huduma za Meli nchini (MSCL) Erick Hamis akizungumza kwenye hafla ya utiaji saini wa mikataba ya ukarabati wa meli tatu
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Huduma za Meli Erick Hamis (Kulia) akisaini mikataba ya ukarabati wa meli tatu .
Wananchi na viongozi mbalimbali waliohudhuria hafla ya utiaji saini wa mikataba ya ukarabati wa meli tatu na uzinduzi wa meli ya Mv Umoja
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Bodi na menejimenti ya Huduma za meli (MSCL) wametakiwa kusimamia kikamilifu Miradi inayotekelezwa na serikali ili kuhakikisha fedha inayogharamiwa na walipa Kodi inaleta thamani.
Maagizo hayo yametolewa leo Jijini Mwanza na Naibu Waziri wa uchukuzi David Kihenzile katika hafla ya utiaji Saini mikataba ya ukarabati wa meli tatu itakayogharimu sh, Bilioni 48.092 pamoja na uzidunzi wa meli ya Mv Umoja iliyogharimu Sh, Bilioni 21.
David ameeleza kuwa kusainiwa kwa miradi hiyo mitatu imelenga kukidhi mahitaji ya usafiri Kwa abiria hususani katika ziwa Tanganyika na kutumia fursa zilizopo katika kuhudumia masoko ya Nchi jirani.
“Ukarabati wa meli ya kubeba abiria na mizigo ya MV Liembe itasaidia kurejesha huduma ya usafiri wa abiria na mizigo, meli MT Nyangumi itasaidia usafirishaji wa shehena ya mafuta kuelekea Nchi ya Uganda na Sudan ya kusini, pamoja na Meli ya MT Ukerewe itakuwa ni msaada mkubwa kwa ajili ya shughuli za uokozi katika ziwa Victoria wakati wa dharura” alisema Kihenzile.
Amefafanua kuwa ukarabati wa meli hizo utawasaidia wakazi wa mwambao wa ziwa Tanganyika pamoja na Nchi za jirani za DRC, Burundi na Zambia, hivyo na serikali imeweza kuonesha kuwa wameanza kuleta mapinduzi katika sekta ya usafiri Kwa njia ya maji.
Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Amina Makilagi akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Amos Makalla ameeleza kuwa usafiri wa njia ya maji ni tegemeo Kwa wakazi wa Kanda ya Ziwa na ni kichocheo kikubwa Kwa wananchi wa ukanda huo katika kukuza uchumi.
Makilagi amefafanua kuwa ujio wa meli hiyo ya MV Umoja itakuwa ni chachu kwa watanzania pamoja na kuleta matokeo chanya yenye tija katika kukuza uchumi wa Mkoa wa Mwanza na ukanda wa ziwa Victoria na Taifa kwa ujumla.
“Hii inatokana na usafiri wa meli kuwa na bei rahisi ya usafiri ukilinganisha na usafiri mwingine wote ni mashahidi kwa wale tunaosafiri” Amesema Makilagi.
Mkurugenzi mtendaji wa huduma za meli (MSCL) Erick Hamis, amesema kuwa meli ya MV Umoja kabla ya ukarabati ilikuwa inabeba mabehewa 19 na baada ya ukarabati inauwezo wa kubeba mabehewa 22 na tani 1200 ya mizigo.
“Meli hii tayari imeanza kutoa huduma kati ya Mwanza na Bandari za Uganda na hivyo kufungua usafirishaji wa shehena ya mizigo kupitia ushiroba wa kati kuelekea Nchini Uganda na Sudan ya kusini” Alisema Hamis.
Meli ya kubeba mizigo ya MV Umoja inayobeba shehena ya mizigo katika ziwa Victoria imefanyiwa ukarabati mkubwa uliogharimu kiasi Cha Dola za kimarekani 8,422,840 ambazo ni sawa na sh, 19,811,446,192 za Kitanzania.