Na. Jacob Kasiri – Arusha.

Mkuu wa Wilaya ya Monduli Mhe.Joshua Nassari amesema kuwa Kampuni ya Kitalii ya African Zoom imejitosa na kukubali masharti na vigezo vilivyowekwa na TANAPA katika zoezi la kuwapandisha watanzania kusheherekea maadhimisho ya miaka 62 ya Uhuru wa Tanzania Bara kwa kupandisha Bendera ya Taifa katika Kilele cha Mlima Kilimanjaro almaarufu “Uhuru Peak”, kama alivyofanya Kapteni Alexander Gwebe Nyirenda tarehe 9.12.1961.

Mhe. Nassari ameyasema hayo wakati wa uzinduzi wa kampeni ya Twenzetu Kileleni Msimu wa 3, iliyofanyika leo tarehe 10.11.2023 katika ofisi za Kampuni ya African Zoom zilizopo Njiro jijini Arusha.

Katika uzinduzi huo, Mhe.Nassari alisema, “kampeni hii iwe chachu kwa watanzania wengi kujitokeza na kuhamasika kupanda mlima huu ambao ni mrefu kuliko yote barani Afrika”.

Aidha, Mhe. Nassari aliongeza kuwa zoezi la kupanda Mlima Kilimanjaro kuadhimisha miaka 62 ya Uhuru wa Tanganyika litatujengea uzalendo, umoja, ushirikiano na mshikamano hivyo ni muhimu sana tushiriki kwa pamoja.

Mhifadhi Daraja la Kwanza – TANAPA Evance Magomba aliipongeza Kampuni ya African Zoom kwa kujitosa kupandisha watanzania katika Kilele cha Mlima Kilimanjaro kuadhimisha miaka 62 ya Uhuru wa Tanzania Bara.

Mhifadhi huyo alisema, “TANAPA imeboresha miundombinu wezeshi ili kuwarahisishia watalii zaidi ya 300 wanaotarajia kujitosa katika zoezi hili la Twenzetu Kileleni ili kutimiza adhma yao ya kufika katika kilele kirefu zaidi barani Afrika bila kikwazo chochote”.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Kitalii ya African Zoom Magret David alisema, “Tumefarijika sana kupata nafasi hii ya kuwapandisha watanzania wenzetu juu ya Paa la Afrika, niwaahidi safari yenu itakuwa ya mafanikio makubwa. Safari yetu itaanzia Lango la machame tarehe 04.12.2023 na kuhitimishwa katika Lango la Marangu tarehe 10.12.2023”.

“Kwa njia ya Machame tutalala kwenye mahema tofauti na njia ya Marangu, hivyo niwasihi watanzania kupanda nasi kampuni ya African Zoom ili muonje radha nzuri naya tofauti ya kulala kwenye mahema” aliongeza, Mkurugenzi huyo.

Zoezi la “Twenzetu Kileleni 2023”, lenye Kaulimbiu “Tunza Mazingira ya Ukanda wa Pwani Okoa Barafu ya Mlima Kilimanjaro” kwa mwaka huu litatumia njia 3 ambazo ni Machame, Londolosi na Marangu huku kampuni 3 za utalii ambazo ni African Zoom, African Scenic na Zara Tours zikipewa dhamana na TANAPA ya kuwapandisha watanzania tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma.