Na Mwandishi wetu, Babati
SHULE ya awali na msingi Tarangire iliyopo Wang’waray Wilayani Babati Mkoani Manyara, imefanya mahafali ya tano ya wanafunzi wake kuhitimu darasa la saba.
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Juma Amma akizungumza kwenye mahafali hayo amesema wanafunzi 25 wamehitimu darasa la saba.
Mwalimu Amma amesema kati ya wahitimu hao 25 wasichana ni 12 na wavulana ni 13.
Amesema shule hiyo ilianzishwa Septemba 26 mwaka 2016 ikiwa na wanafunzi 12 walimu 2 na watumishi wasio walimu 5.
“Shule ilikuwa na majengo 14 ikijumuisha madarasa, vyoo vya kike, vya kiume, jiko, stoo, mabweni na jengo la utawala,” amesema mwalimu Amma.
Amesema shule hiyo ina jumla ya wanafunzi 362 wanaosoma kuanzia shule ya awali, darasa la kwanza hadi la saba.
Amesema kati ya wanafunzi hao 362 waliopo shule ya awali ni 76, shule ya msingi ni 292 na wasichana ni 183, wavulana ni 176.
Katibu Tawala Msaidizi Mkoa wa Manyara (Utawala) Dominick Mbwette amewapongeza, wanafunzi, walimu, wazazi na viongozi wa shule hiyo kwa kufanya mahafali ya tano tangu ianzishwe.
“Nawapongeza kwa hatua hii kwani siyo ndogo, ila msibweteke ongezeni juhudi katika kuhakikisha shule hiyo inazidi kupiga hatua ya maendeleo,” amesema Mbwette.
Hata hivyo, amewataka wanafunzi waliohitimu darasa la saba wahakikishe wanaendelea na elimu ya sekondari kwani huo ni mwanzo wa safari ndefu ya elimu.