Mtaalamu wa kilimo wa kampuni ya mbegu ya Corteva Agriscience, Fikiri Abel akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na mbegu hizo mpya za mahindi na dawa za kuua wadudu na magugu shambani.
Julieth Laizer,Arusha .
Wakulima wameshauriwa kutumia mbegu mpya za mahindi ambazo zinastawi kwa wingi na kufanya vizuri katika ukanda wa kati na wa chini na kuweza kupata mavuno zaidi.
Hayo yamesemwa jijini Arusha katika viwanja vya maonyesho ya nanenane Themi Njiro na Mtaalamu wa kilimo kutoka kampuni ya mbegu ya Corteva Agriscience ,Fikiri Abel wakati akitoa elimu ya matumizi ya mbegu mpya za kilimo kwa wakulima walipotembelea katika banda lao lililopo nanenane.
Fikiri amesema kuwa,kampuni hiyo imekuja na mbegu mpya za kilimo aina mbili ambazo zinavumilia hali mbaya ya hewa ambazo ni Pan 53 ambayo inafanya vizuri ukanda wa kati na inakomaa ndani ya siku 90 na kutoa magunia kuanzia 35 hadi 40 kwa ekari .
Ametaja mbegu nyingine kuwa ni Pan 3m-05 ambayo inafanya vizuri ukanda wa chini na inakomaa ndani ya siku 75 na inatoa magunia 25 hadi 30 kwa ekari .
Aidha Fikiri amesema kuwa,wamefikia hatua ya kuja na mbegu mpya na bora kwa kilimo kwa msimu huu wa nanenane ili wakulima waweze kuvunja mahindi mengi zaidi na kuweza kuzalisha kwa kiwango cha juu kutokana na hizo mbegu bora za kisasa.
“Mbegu hizi zimezingatia mahitaji ya mkulima na sehemu anayolima kwani tayari zimefanyiwa utafiti wa kutosha ambao unamwezesha mkulima kuwa na uhakika wa kilimo chake na kuweza kulima kilimo chenye tija na manufaa kwake na Taifa kwa ujumla.”amesema Fikiri .
Aidha amesema kuwa, wamekuja na dawa nzuri ya kuua wadudu wanaoshambulia mahindi pamoja na dawa ya kuua magugu shambani ambapo kampuni hiyo imekuja na sumu inayodhibiti mdudu vizuri na kumwezesha mkulima kutorudia kuweka dawa mara kwa mara.
Amefafanua kuwa,wakulima wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya kutumia mbegu mbalimbali za mahindi na wamekuwa hawaambulii chochote badala yake wanaishia kupata hasara tu ,ambapo amewataka kutembelea katika banda la Corteva Agriscience na kuweza kujionea mbegu bora za mahindi ili asipate hasara wakati kuna mbegu bora na za uhakika kwa ajili yao.