Na Mwandishi wetu, Mirerani
MWENYEKITI wa CCM Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, Kiria Ormemey Laizer, amezindua rasmi mashindano ya Polisi Jamii Cup 2023 Mirerani yanayofanyika katika viwanja vya Tanzanite Complex Stadium (kwa Mnyalu) Mji mdogo wa Mirerani.
Kiria akizungumza kwenye ufunguzi wa michuano hiyo amewapongeza polisi kwa kuanzisha michezo hiyo ambayo kwa namna moja au nyingine itakuwa kichocheo cha burudani.
Amewataka vijana kupenda kushiriki kwenye michezo kwani michezo huimarisha afya, ajira na kujenga ushirikiano na mshikamano kwa jamii inayowazunguka.
“Michezo pia ni utekelezaji wa ilani ya uchaguzi wa CCM hivyo tunawapongeza viongozi wa polisi hususani OCS Mirerani kwa kuanzisha jambo hili zuri na la kupongezwa kwa vijana wapenda michezo,” amesema Kiria.
Mkuu wa kituo cha polisi mirerani, Mrakibu wa polisi (SP), Dominick Fwaja akizungumza kwenye michuano hiyo, amesema mashindano hayo yana lengo la kupinga vitendo vya ukatili na matukio mengine ya uhalifu eneo hilo.
OCS Fwaja amesema kwa kupitia falsafa ya Polisi Jamii itasaidia kuiweka jamii karibu na polisi, jambo litakalowezesha kupata taarifa za uhalifu kwa urahisi na kuwaondoa wananchi hofu iliyojengeka kwa polisi.
Amesema wameandaa mashindano hayo ikiwa ni utaratibu uliopo chini ya IGP Camillus Wambura lengo likiwa kutoa elimu juu ya tabia hatarishi na vijana kuwa na afya bora kupitia michezo hivyo kuwaepusha vijana kuacha tabia za matumizi ya dawa za kulevya, bangi na ulevi ambavyo huchangia kuzorotesha uchumi wa nchi.
Mwenyekiti wa chama cha soka wilaya ya Simanjiro (SIDFA), Charles Mnyalu amewapongeza polisi kwa kuanzisha michuano hiyo ambayo itachangia vijana kushiriki michezo.