Na Fauzia Mussa, Maelezo                                 

Wakala wa Chakula na dawa Zanzibar (ZFDA) wamewataka wafanyabiashara kutokujaza bidhaa katika makontena na badala yake kuwacha nafasi ya kuweza  kuruhusu hewa kuingia ili kuepusha kuharibika kwa bidhaa kunakosababishwa na joto.

Wito huo umetolewa na Afisa kutoka wakala wa Chakula na Dawa (ZFDA)Mohammed Shauri wakati walipofika katika ghala la  kampuni ya Sahal Geaneral Store liliopo Malindi  kwa ajili ya ukaguzi na kugundua tani zaidi ya  mia moja za Mchele zilizoingizwa kutoka Pakistan  zimeharibika  kwa kubadilika rangi na kuingia wadudu ,hivyo mchele huo umezuiliwa kwa matumizi ya Binaadamu.
Akielezea sababu zilizopelekea kuharibika kwamchele huo amesema ni pamoja  na joto lililochangiwa na ujaaji wa Bidhaa hiyo na kukaa sana kwenye makontena kulikotokana na uzorotaji wa ufuataji wa taratibu za Bandari kwa Wafanya Biashara.
“niwashauri Wafanya Biashara kufuata taratibu  mapema ili kuepusha bidhaa zao kukaa muda mrefu ndani ya makontena kunakopelekea kuharibika kwa bidhaa hizo na kusababisha hasara kwao na madhara kwa jamii”. alishauri  Afisa huyo
Aidha amewaomba Wafanya biashara kuacha kuingiza bidhaa  masokoni mara tu wanapoona dalili za kuharibika kwa bihaa hizo na badala yake kufika ZFDA kwa ajili ya ukaguzi  ili kuepusha  madhara   yanayoweza kuepukika.
Mapema Afisa kutoka  ZFDA aliitaka kampuni ya Sahal General Store kufuata taratibu watakazopewa na ZFDA ili kuuteketeza Mchele huo  kwani unaweza kusababisha madhara makubwa  kwa jamii.
Kwa upande wake  Mkuu wa utoaji wa  mizigo Bandarini katika kampuni ya Sahal General Store Juma Abubakar Alhaji amesema kuharibika kwa mchele huo kumechangiwa na joto lililosababishwa na ukaaji wa muda mrefu Bandarini ,hivyo ameiomba Serikali kuboresha miundombinu ya Bandari ili kuepusha msongamano wa meli za makontena Bandarini kunakopelekea kuchelewa kushushwa kwa makontena.
Aidha bwana Juma amesema wapo tayari kushirikiana na Wakala wa Chakula na Dawa Zanzibar kuhakikisha mchele huo hautumiwi na binaadamu kwani wapo kwaajili ya kulinda Afya za Binaadamu na sio kuwaangamiza.  
Ukaguzi wa ZFDA umefanyika kufuatia kampuni ya Sahal General Store kujisalimisha mara baada ya kuhisi mchele huo walioingiza  haufai kwa matumizi ya Binaadamu .