Kaimu Meneja wa TMDA kanda ya kaskazini,Dk Furaha Nyunza akizungumza kwenye semina hiyo jijini Arusha .
Mkurugenzi wa taasisi ya Reepads Sanitary Products ,Rephrin Kombe akizungumza katika semina hiyo jijini Arusha.
Mkuu wa kitengo cha ukusanyaji wa mapato ya ndani kutoka TEMDO ,Elisha Sibale akizungumza katika semina hiyo.
*******************
Julieth Laizer ,Arusha.

Arusha.MAMLAKA  ya dawa na vifaa tiba (TMDA) kanda ya kaskazini imetoa elimu kwa wadau wa  utengenezaji uingizaji na usambazaji wa dawa vifaa tiba na vitendanishi kuhusu sheria ya dawa vifaa tiba sura no .219 pamoja na kuwafanya wafanye biashara zao kwa kuzingatia sheria na miongozo  mbalimbali. 

Hayo yamesemwa na Kaimu Meneja wa TMDA kanda ya kaskazini ,Dk Furaha Nyunza wakati akizungumza na wadau hao katika mafunzo hayo yaliyofanyika jijini Arusha.
Dk.Nyunza amesema kuwa,lengo la mafunzo hayo ni kuweza kuwakumbusha wajibu wao katika kuwahudumia wananchi sambamba na kuweza kujadili changamoto mbalimbali  zilizopo katika biashara ya dawa vifaa tiba na vitendanishi na kuweza kutafutia muafaka wake.
Amesema kuwa,baada ya mafunzo hayo wanatarajia wadau hao watafanya  kazi zao kwa ufanisi mkubwa pamoja na kuweza kupunguza bidhaa bandia ambazo vimekuwa vikihatarisha afya ya jamii .
“TMDA ni taasisi iliyochini ya wizara ya Afya maendeleo ya jamii jinsia wazee na watoto yenye jukumu la kulinda afya ya jamii kwa kudhibiti usalama ,ubora na ufanisi wa dawa, vifaatiba na vitendanishi”amesema .
Nao baadhi ya washiriki wa mafunzo  hayo Mkurugenzi wa Taasisi ya kutengeneza pedi ya Reepads Sanitary Products,Rephrin Kombe amesema kuwa ,mafunzo hayo ni ya muhimu sana kwao kwani watawasaidia kufanya biashara yao kwa kufuata sheria za mamlaka hiyo .
“Kuna watu wamekuwa wakifanya  biashara zao bila kufuata taratibu za mamlaka hiyo hali ambayo imekuwa ikihatarisha  afya za walaji  kwa kutengeneza bidhaa feki hivyo ni vizuri wakafika katika ofisi za mamlaka hiyo na kuweza kupata taratibu  za kufuata.”amesema.
Mdau mwingine  kutoka Taasisi ya usanifu na uhandisi mitambo(TEMDO),Mkuu wa kitengo cha ukusanyaji wa mapato ya ndani ,Elisha Sibale amesema kuwa,wakiwa kama wadau wanaojihusisha na uzalishaji wa vifaa tiba mafunzo hayo kwao ni muhimu sana kwani yatawawezesha kutoa huduma kwa jamii kwa kufuata sheria na taratibu zilizopo hivyo ni jambo zuri kuendelea  kukumbushana.