MKUU wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule,akizungumza na waandishi wa habari leo Februari 24,2023 jijini katika Mwendelezo wa Programu maalumu ya kuelezea mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita ndani ya kipindi cha miaka miwili katika Hospital ya Benjamin Mkapa Dodoma .

Mkurugenzi Mtendaji wa I Hospital ya Benjamin Mkapa (BMH) Dkt. Alphonce Chandika,,akizungumza wakati wa kuelezea mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita ndani ya kipindi cha miaka miwili katika Hospital ya Benjamin Mkapa Dodoma .

Na.Alex Sonna-DODOMA

SEKTA ya Afya imeendelea kuimarika na kuongezeka zaidi  Mkoa wa Dodoma katika kipindi cha miaka miwili ya Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa na miundombinu bora ya Vituo vya kutolea huduma za Afya tofauti na kipindi cha nyuma.

Hayo yamesemwa leo Februari 24,2023 jijini Dodoma na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule wakati akizungumza na waandishi wa habari katika mwendelezo wa Programu maalumu ya kuelezea mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita ndani ya kipindi cha miaka miwili katika Hospital ya Benjamin Mkapa Dodoma .

RC Senyamule amesema kuwa katika kipindi cha miaka miwili chini ya Rais Dkt.Samia huduma ya Afya Mkoa wa Dodoma imeendelea kuwa bora kutokana na kuwepo kwa utoaji huduma bora ambao umekuwa ukitolewa na  Hospitali ya Benjamin Mkapa.

”Naipongeza Hospitali ya Benjamin Mkapa kwa kuendelea kutoa huduma mbalimbali kwa wakazi wa Dodoma pamoja na mikoa mingine ambayo imekuwa ikiitengemea Hospitali hiyo ambayo imekuwa ikitoa huduma mbalimbali za Matibabu”amesema RC Senyamule

Amesema kuwa kumekuwa na kituo cha Damu Salama Kanda ya kati kilichopo Mkoani Dodoma, uwepo wa kituo hiki umerahisisha upatikanaji wa damu salama na mazao ya damu.

”Uwepo wa Kituo hicho kimeendelea kusaidia kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi na vifo vya watoto wachanga ikiwa ni pamoja na kupunguza gharama ambazo zilikuwa zinatumika kusafirisha sampuli za damu Kwenda Maabara Kuu ya Taifa iliyopo Dar- es Salaam.”ameeleza RC Senyamule

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa I Hospital ya Benjamin Mkapa (BMH) Dkt. Alphonce Chandika,amesema kuwa wamefanikiwa kupandikiza figo kwa watu 31 na kuokoa fedha kiasi cha zaidi ya shilingi bilioni 2.3.

Dkt. Chandika amesema katika kipindi cha miaka miwili cha Serikali awamu sita Hospitali ya Benjamin Mkapa imepiga hatua kubwa sana imefanikisha kuimarisha kwa huduma ya upandikizaji wa Figo kwa idadi ya Wagonjwa 31 na kuendelea vizuri na afya zao.

”Tumefanikiwa kuanzisha huduma za upandikizaji wa figo na jumla ya wananchi 31 wamenufaika na huduma hiyo, huku gharama ya huduma hiyo ikiwa ni takriban shilingi milioni 25 wakati India  angetibiwa kwa takriban Shilingi milioni 100 ambapo kwa wagonjwa hao 31, Serikali imeokoa zaidi ya Shilingi bilioni 2.3”amesema Dk.Chandika

Amesema kuwa Hospitali hiyo imefanikiwa kutoa huduma za matibabu ya moyo ambapo kuna maabara maalum inayotumika katika kutoa matibabu ya moyo pasipo kufungua kifua.
“Hospitali hii ni ya pili hapa nchini kutoa huduma hii.Tangu huduma hii imeanza kutolewa mwaka 2019, jumla ya wananchi 715 wamehudumiwa kwa kuchunguzwa,”Amesema Dkt.Chandika
Amesema kuwa wagonjwa 39 waliobainika kuwa na matatizo makubwa ya moyo wamehudumiwa kwa kuwekewa vipandikizi na kati ya 39, wagonjwa wawili kati yao walihudumiwa kwa dharura ambapo kama ingekuwa ni kusafirishwa kwenda kupatiwa matibabu Dar es Salaam wangepoteza maisha.
“Kuna wagonjwa nane ambao mapigo yao ya moyo yanashuka sana, walihudumiwa katika Hospitali ya Benjamin Mkapa kwa kupandikizwa betri kwenye moyo na kupitia maabara hiyo tumeweza kuhudumia watoto 14 waliozaliwa na matatizo ya moyo,”Amesema Dkt.Chandika
Na kuongeza kuwa “Hospitali imeanza kufanya upasuaji wa moyo kwa watoto waliobainika kuwa na matatizo ya kuzaliwa ya moyo ambapo tayari watoto kumi wameshahudumiwa,”Amesema Dkt.Chandika
Pia tangu mwaka 2020, Hospitali ilifanikiwa kuanzisha upasuaji wa nyonga na magoti kwa kuweka vipandikizi, hadi sasa jumla ya wagonjwa 56 wamewekewa vipandikizi hivyo kwa wastani wa gharama ya shilingi milioni 12. Gharama za huduma hii nchi za nje ni takriban milioni 35 ambapo kwa wagonjwa 56 waliohudumiwa , Serikali imeokoa jumla ya Shilingi bilioni 1.28
“Hospitali hii ndio pekee nchini imefanikiwa kuanzisha huduma ya uvunjaji wa mawe kwenye figo kwa kutumia mawimbi na miale pasipo kumfanyia mgonjwa upasuaji, huduma hii imeshatolewa kwa wagonjwa 148 kwa gharama ya Shilingi milioni 1.2 kwa mgonjwa mmoja, kwa nje ya nchi gharama ni zaidi ya milioni 7 ambapo kwa wagonjwa 148, Serikali imeokoa zaidi ya Shilingi milioni 850,”Ameeleza Dkt.Chandika
Katika jitihada za Serikali kuhakikisha inawaletea wananchi huduma za afya zilizo bora, ilidhamiria kuiwezesha Hospitali ya Benjamini Mkapa kuwa na vifaa tiba vya kisasa na vinavyotumia teknolojia ya kisasa ili iweze kukidhi adhma yake ya kuwahudumia wananchi kwa kuwapatia matibabu ya kiwango cha juu.

Dkt.Chandika amesema kwa mwaka 2022/23 hospitali hiyo imeanza ujenzi wa kituo cha mionzi cha matibabu ya saratani ambapo wamepokea Sh.Bilioni 10.

”Serikali inaendelea kutekeleza mrandi mingine katika Hospitali ya Benjamini Mkapa kwa kujenga Jengo la Mionzi Tiba unaogharimu Shillingi Billioni 28 na Serikali imetoa Shillingi 2.9 kwa malipo ya awali kwa Mkandalasi na Ujenzi umefikia asilimia 15.6%.”amesema  Chandika