Naibu waziri wa nchi ofisi ya Rais utumishi wa umma ,Deogratius Ndejembi akizungumza katika kikao kazi cha 3 cha serikali mtandao kinachofanyika jijini Arusha.

Washiriki wa kikao hicho  kilichoandaliwa na Mamlaka ya serikali mtandao  kutoka mikoa mbalimbali kinachoendelea jijini Arusha. 

Katibu Mkuu ofisi ya Rais utumishi ,Laurian Ndumbaro akizungumza katika kikao hicho jijini Arusha leo.
**********************
Julieth Laizer,Arusha.
Arusha.Naibu waziri wa nchi ofisi ya Rais utumishi wa umma ,Deogratius Ndejembi amezitaka taasisi zote za umma nchini kuendana na kasi ya mabadiliko kwa kufanya shughuli zake kwa kutumia mfumo wa Tehama.
Ameyasema hayo leo jijini Arusha wakati akifungua kikao kazi cha 3 cha serikali mtandao  kilichoandaliwa na Mamlaka ya serikali mtandao (eGA)  kilichowashirikisha watumishi wa umma kutoka mikoa mbalimbali ,huku kauli mbiu ikiwa ni “Mifumo jumuishi ya TEHAMA kwa utoaji bora  wa huduma za umma.”
Amesema kuwa,utoaji wa huduma kwa  taasisi za umma kutumia mfumo wa Tehama bado zipo chini hivyo ni wakati sasa wa kuhakikisha taasisi hizo zinatumia mfumo huo kuwafikishia wananchi wake huduma ili kuendana na kasi ya mabadiliko. 
Ndejembi amewataka wakuu wote wa taasisi za umma kuhakikisha wanajiunga na mfumo  huo ili kuendana na kasi ya  Rais Samia Suluhu Hassan  ya kutaka huduma zote zifikie wananchi kupitia mfumo wa  kidigitali. 
“Niwaombe pia mhakikishe mnapeleka huduma karibu na wananchi kupitia mfumo wa Tehama ili kuwarahishia wananchi kupata huduma hizo kwa haraka na kwa wakati  “amesema Ndejembi. 
Amefafanua kuwa, endapo taasisi nyingi zitautumia  mfumo huo zitasaidia  sana kuondoa urasimu  kwa kutumia makaratasi kwani shughuli nyingi duniani  hivi sasa  zinatolewa  kwa kutumia  Tehama na zimefanikiwa kwa kiwango kikubwa sana.
Aidha alitoa wito pia kwa taasisi binafsi nazo kujitahidi  kutumia mfumo huo wa serikali mtandao kwani una manufaa makubwa katika utoaji wa huduma kwa wananchi .
Katibu  Mkuu ofisi ya Rais utumishi  ,Laurian Ndumbaro amewataka wakuu wa taasisi kujitahidi kubadili  website  zao  ili ziendane kisasa ,huku akitaka vikao mbalimbali vya bodi  vinavyofanyika  kuhakikisha vinafanyika kidigitali. 
“Ifike wakati sasa hata baraza la madiwani  ,vikao  mbalimbali vya halmashauri na katika majiji  zifanyike kidigitali ili serikali yetu iwe serikali ya mtandao  na tuhakikishe tunashuka  hadi  huko chini kwa wananchi wote .”amesema Ndumbaro. 
Naye Mkurugenzi wa  Mamlaka ya serikali mtandao (eGA) ,Mhandisi Benedict Ndomba amesema kuwa,wamekuwa  wakifanya kazi zao kwa weledi ,ubunifu,na ushirikiano pamoja na kufanya kazi kwa pamoja katika kutoa elimu kuhusu serikali mtandao. 
Amesema kuwa,wamekuwa  wakifanya ukaguzi wa mifumo na miundombinu ya Tehama ambapo mamlaka hiyo imeweza kusimamia kikamilifu miundombinu ya mtandaoni.
Aidha ametaja  changamoto  wanazokabiliana nazo kuwa ni pamoja na upungufu wa  wataalamu wa Tehama ambapo wadau wa serikali mtandao kupitia kikao hicho kwa pamoja wataweza kuweka mikakati namna ya kukabiliana na changamoto  hizo.